Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika kijiji cha Ukange kata ya Lupila wilayani Makete mkoani Njombe wameipongeza TASAF kwa kuwapa mradi wa kilimo cha umwagiliaji wenye thamani ya mil 71 ambao wamedai kuwa tangu waanze kutekeleza mradi huo umekuwa na matokeo chanya katika maisha yao.
Mradi huo ambao unatekelezwa kupitia kikundi cha wanufaika 71 wa mpango umetajwa kuimarisha kipato kwa wanufaika na wanakijiji wanaofanya kilimo cha umwagiliaji katika kata hiyo kwa kuwa wamekuwa wakifanya shughuli za kilimo cha viazi ,bustani na nyingine nyingi katika chote cha mwaka hatua ambayo inawapa uhakika wa mlo pamoja ujenzi wa nyumba za kuishi , kusomesha watoto na mambo mengine.
Stelia Sanga ni mmoja wa wanufaika wa mpango wa TASAF katika kijiji cha Ukange akizungumzia hali ya maisha ya familia yake ilivyokuwa awali kabla ya kuanza kupata fedha za mpango huo amesema maisha yake yalikuwa duni kiasi ambacho hakuwa na uhakika wa milo mitatu na kuishi katika nyumba ya nyasi.
“Kabla ya kuanza kutambuliwa na TASAF maisha yangu na familia yangu yalikuwa sio kitu ,sikua na uhakika wa chakula na kuishi katika nyumba ya nyasi hivyo tangu nianze kupokea fedha hizi niliweka malengo na kuanza kudunduliza mpaka nikajenga “alisema Sanga.
Kuhusu matokeo chanya ya kuanzishwa kwa mradi wa umwagiliaji kijijini hapo ambao umetolewa na TASF Maltin Msigwa ambaye pia ni mnufaika amesema umeweza kumuongezea kipato hatua ambayo imemfanya na yeye kuanza kufanya kilimo cha viazi katika shamba la ekari moja na nusu na pia kuweza kujenga nyumba ya kuishi pamoja na ufagaji wa kuku na mbuzi hatua ambayo ilikuwa ni ngumu kufanyika awali.
Kufuatia mafanikio hayo kuletwa na mradi huo wakazi wa kijiji cha Ukange wanashindwa kuzuia hisia zao kwa serikali ya awamu ya tano kwa kuwapa mradi huo na kuomba kuendelea kuwapa nafasi ya upendeleo endapo ukiendelea ili waweze kuondokana na wimbi la umasikini.
Mbali na hilo kijiji hicho ambacho kimekuwa kikifanya kilimo cha viazi mviringo kwa wingi kimetoa rai kwa serikali kuwatafutia masoko ya viazi ili kuepusha unyonyaji mkubwa unaofanywa na wafanyabiashara na walanguzi ambao wamekuwa wakinunua viazi kwa debe badala ya kilo na kuwanyonya ambapo wamesema kwa wastani kila debe moja wamekuwa wakinunua shilingi elfu 2 badala ya elfu 7 jambo ambalo linawatia hasara kubwa.
Unyonyaji huo unawafanya kupaza sauti kwa serikali kuanzisha vituo vya pamoja vya biashara ili kuwa na sauti ya pamoja ya bei pamoja na viwanda vya kuongeza thamani mazao yao ili kutengeneza faida.
Kufuatia wakulima kutoa kilio hicho kwa serikali mtandao huu unapiga hodi kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wiilaya ya Makete Fransis Namaumbo ambaye anaeleza jitihada ambazo zimeendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja uimarishaji wa vyama vya ushirika ili kuvitumia kama kituo cha biashara ya malighafi ama bidhaa wanazozalisha.
Namaumbo amesema serikali iko katika maboresho ya barabara za kuelekea masokoni kwa kiwango cha lami hatua ambayo itamfanya mkulima kusafirisha mazao yake mpaka masokoni na kuuza kwa faida huku pia akidai kuwa taratibu za kuanzisha maghala zimeanza.
“Tunashukuru serikali ya awamu ya tano imeanza ujenzi wa barabara ya Njombe hadi Makete Kwa Kiwango cha Lami pamoja kuvijengea uwezo vyama vya ushirika ili vitumike na wakulima kama vuto vyao vya biashara ili kudhibiti unyonyaji unaofanywa na wafanyabiashara” alisema Fransis Namaumbo.
Nae Jakrin Mlosso ambaye ni mratibu wa TASAF katika halmashauri ya wilaya ya Makete akieleza sababu ya kutoa mradi wa umwagiliaji katika kijiji cha Ukange anasema ni kutokana na wakazi wake kujikita zaidi katika shughuli za kilimo.
Kuhusu kiwango cha fedha kilichotolewa kutekeleza miradi tangu 2015 hadi sasa Mlosso anasema ni bil 2.5 ambazo zimetumika kutekeleza miradi 39 kutoka sekta ya afya,elimu,barabara na nyinginezo huku nae afisa maendeleo kata ya Lupila Veronica Kalimba akidai mpango huo wa kunusuru kaya Masikini umeleta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha udumavu.