Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na Uongozi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar leo wametembelea Bohari ya Dawa (MSD) kubadilisha uzoefu katika masuala ya mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Bi. Mwanaasha Khamis Juma amesema hivi karibuni Zanzibar wamepitisha sheria ya kubadili utendaji wa Bohari Kuu ya Dawa ya Zanzibar, ambapo mabadiliko hayo ni moja ya sababu iliyowafanya kuja kutembelea MSD.
“Ujio wetu hapa tumeona ukubwa na ufanisi wa MSD hasa kwenye majukumu yake ya uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya nchini. Tuemetembelea ghala la kuhifadhi dawa ni ghala kubwa na linalotumia mifumo ya kisasa ya utunzaji wa bidhaa za afya” Amesema Mhe. Mwanaasha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Bw. Mavere Tukai amewaeleza Wawakilishi hao kuwa MSD kwa sasa ni kati ya taasisi zilizowekwa kwenye kundi la taasisi za kimkakati, yaani taasisi ambazo zinatakiwa kujiendesha kibiashara au kujitegemea zenyewe.
“Mmekuja kipindi kizuri ambapo MSD inafanya maboresho mbalimbali ili kuhakikisha inatekeleza azima hiyo ya serikali ya kujiendesha kibiashara”. Alisema Tukai.