Katibu Mkuu Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Khamis Abdalla Said (katikati), naibu Mkurugenzi KOICA Tanzania Jieun Seong (kushoto) na meneja mradi wa UNOPS John. Bundu Fofanah (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja katika hafla ya makabidhiano ya maabara za kisasa na vifaa baina ya Wizara ya elimu na Serikali ya jamuhuri ya korea kupitia shirika la Koica huko skuli ya Machui Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar Lela Muhammed Mussa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha maabara skuli ya Machui ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari Zanzibar kilichojengwa na wazazi kwa kushirikiana Koica .
Katibu Mkuu Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Khamis Abdalla Said akizungumza jambo na waziri wa wizara hiyo pamoja na watendaji wa shirika la Koica wakati wa kitembelea maabara ya Skuli ya machui katika makabidhiano ya mabara hizo ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar Lela Muhammed Mussapamoja na viongozi mbalimbali wakitembelea miongoni mwa maabara zilizojengwa na shirika la Koica ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari Zanzibar,huko Machui Mkoa wa kusini Unguja. (PICHA NA MPIGA PICHA WETU)
…….
Na Imani Mtumwa , Maelezo
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe,Lela Mohammed Mussa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kuimarisha maendeleo ya kielimu Nchini.
Akizungumza katika makabidhiano ya maabara za kisasa zilizojengwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi, kwa ushirikiano wa Korea (KOICA) huko Skuli ya Sekondari Machui Wilaya ya Kati Unguja amesema makabidhiano hayo ni utekelezaji wa mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari Zanzibar.
Aidha amesema Shirika la KOICA ni moja kati ya Shirika linalo unga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuboresha Miundo mbinu mbali mbali hasa katika sekta ya Elimu.
Hata hivyo amesema Wizara itasimamia kwa karibu ili kuhakikisha Vifaa vya Maabara vinapatikana kwa Awamu na kutuzwa vizuri kwa matumizi ya Maabara hizo.
Vile vile ameeleza, kuwepo kwa Maabara za kisasa Unguja na Pemba kutasaidia wanafunzi kusoma vizuri kwa vitendo na kuleta matokeo chanja katika masomo ya Sayansi.
Aidha aliwataka wazazi wa eneo hilo kujua majukumu na wajibu kwa watoto wao na kuhakikisha Wanafunzi wanasoma vizuri ili kuweza kuendeleza elimu Nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Khamis Abdullah Said amelishukuru Shirika la Koica kwa kuwapatia uwezo Walimu zaidi 1300 katika ufundishaji wa masomo ya Sayansi.
Aidha, amewataka wanafunzi kuzitumia vyema Maabara hizo pamoja na kusoma kwa bidii ili kufikia lengo lililokusudiwa .
Akisoma Risala Mkurugenzi wa Koica nchini Tanzania Bw. Jieun Seong amesema Mradi huo wa kuboresha Maabara za kisasa umeanza Mwezi January 2020 na kumalizika Mwezi wa Septemba 2023.
Amesema Jumla ya shiling Milioni 3 USD Dolar, zimetumika mpaka kukamilika kwa Mradi huo wenye lengo la kuboresha Sekta ya Elimu katika nyanja ya Masomo ya Sayansi
Amesema, Jumla ya Maabara zilizo jengwa ni kumi kwa Unguja na Pemba. ikiwemo Bubwini, Fukuchani, Jendele, Machui, na Jongowe Sekondari Skuli kwa Unguja na Chambani, Chanjamjawiri, Shumba, Uondwe na Wambaa kwa Upande wa Pemba.
Nao baadhi ya wazazi na walezi wamesema wataungana pamoja na Serikali kwa kutoa ushirikiano wao ili kuhakikisha watoto wao wanasoma na kuvitumia vifaa vya maabara hiyo ili kukuza sekta ya elimu katika jamii.