………..
Na Muhidin Amri,
Tunduru
KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali kukuza na kuboresha sekta ya elimu hapa nchini,Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu)kimetoa msaada wa mifuko 20 ya saruji na mchanga lori mbili kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo kwa shule ya kulea watoto ya Hannover Day Care.
Shule hiyo inayomilikiwa na kanisa la Biblia Tanzania,inajihusisha kutoa elimu na malezi kwa watoto wadogo wilayani Tunduru,inakabiliwa na changamoto kubwa ya vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo na ukumbi kwa ajili ya kulia chakula.
Akikabidhi msaada huo kwa mwalimu mlezi na mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo,Meneja mkuu wa Tamcu Iman Kalembo amesemaTamcu imeamua kutoa msaada huo ili usaidie katika ujenzi wa vyoo na madarasa li kuwawezesha watoto wapate sehemu sahihi ya kujifunzia na kujistili.
Kalembo alisema,huo ni mwanzo katika kuhakikisha shule hiyo inakuwa na mazingira bora na rafiki ya kufundishia na kujifunzia na kuwa kimbilio la wazazi wanaotafuta sehemu sahihi kwa ajili ya elimu ya watoto wao na jamii ya wana Tunduru ambao kwa muda mrefu wamebaki nyuma kielimu.
Ametoa wito kwa wadau wengine wakiwemo wazazi wenye watoto wanaolelewa katika kituo hicho kushirikiana na uongozi wa kituo hicho ili kujenga mazingira rafiki ambayo yatawasaidia watoto kukua katika malezi mazuri na kuimarika kitaaluma.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Mchungaji Emmanuel Telela alisema,msaada huo umewafungulia njia kuanza maandalizi ya kufyatua tofali kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo na kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
Amewaomba, wadau mbalimbali wenye moyo na wanaoguswa na changamoto hiyo kujitokeza ili kuwasaidia watoto wanaolelewa katika shule hiyo ili waweze kuboresha mazingira ya shule kwa kuongeza idadi ya madarasa na matundu ya vyoo.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Martha Chowo alisema,saruji waliyopata itasaidia kuongeza idadi ya madarasa na kufanya ukarabati wa vyoo vinavyotumiwa na watoto.
Alisema,katika shule hiyo wanachukua wanafunzi wenye umri kuanzia miaka miwili hadi mitano na kwa sasa wamebaki watoto 13 baada yaw engine 16 kumaliza elimu ya awali miezi miwili iliyopita.