Na Eleuteri Mangi, WANMM
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amekutana na kuzungumza na watumishi wa Wizara hiyo pamoja na watumishi wa Idara ya Ardhi kutoka jiji la Dodoma ambapo amewataka kuwahudumia wananchi kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
Naibu Waziri Pinda amesema hayo Desemba 13, 2023 jijini Dodoma katika kikao cha kuhitimisha huduma za Kliniki ya Ardhi kilichofanyika katika Ofisi za Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma kuanzia Novemba 4 hadi Desemba 12, 2023.
“Onesheni utaalamu wenu, fanyeni kazi kwa vitendo ya kuwahudumia wananchi, badilikeni, fanyeni kazi kwa weledi na tambulikeni kwenye jamii kwa kuwa mfano bora kwa utendaji kazi wenu” amesema Naibu Waziri Pinda.
Aidha, Naibu Waziri Pinda amewataka Wapima Ardhi, Wathamini, Maafisa Mipango Miji pamoja na Maafisa Ardhi kuendelea na moyo wao wa uzalendo waliouonesha wakati wote wa Kliniki hiyo na kuwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma katika maeneo yao ya kazi hata uwandani wanapoenda kuwahudumia wananchi katika maeneo mbalimbali katika jiji la Dodoma.
Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Katibu Mkuu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Antony Sanga amepongeza watumishi hao kwa kufanyakazi ya kutoa huduma kwa Watanzania katika Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. John Kayombo amesisitiza watumishi wa Idara ya Ardhi katika jiji hilo kufanya kazi kulingana na taaluma zao bila kuingilia taaluma ya mtu mwingine kwa kufanyakazi kwa ushirikiano na kuwahimiza wakawe wapya katika kutoa huduma kwa wananchi baada ya kumaliza kliniki hiyo.
“Watumishi wenzangu, tufanye kazi kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatuhitaji kutengeneza migogoro, tunahitaji kutatua migogoro ya ardhi yote iishe, kazi zinatupa heshima” amesema Bw. Kayombo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi hao, Kamishna Ardhi nchini Bw. Nathaniel Mathew Nhonge amesema wamepokea maelekezo ya viongozi na watayatekeleza ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi.