Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe,Othman Masoud Othman akimsikiliza Mtoto Florence Issack akiwa na Mama yake wakati wanaoshughulika na Ujasiria Mali wa Shanga na Kofia wakati akitembelea katika Mabanda ya Wajasiria Mali katika Hafla ya Ufungaji wa Kongamano la Saba la Kiswahili la Kimataifa katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe,Othman Masoud Othman akiangalia Bidhaa ya Majani ya chai na kupatiwa maelezo yake na Mjasiria Mali Mohamed Ally Makame wakati alipotembelea Mabanda ya Wajasiria Mali katika Hafla ya Ufungaji wa Kongamano la Saba la Kiswahili la Kimataifa katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe,Othman Masoud Othman akipokea Zawadi ya Kipepeo na kupatiwa maelezo yake na Mjasiria Mali Jamila Nassor Ali Mkaazi wa Kojani Pemba wakati alipotembelea Mabanda ya Wajasiria Mali katika Hafla ya Ufungaji wa Kongamano la Saba la Kiswahili la Kimataifa katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
Baadhi ya Wageni Waalikwa waliohudhuria katika Hafla ya Ufungaji wa Kongamano la Saba la Kiswahili la Kimataifa katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
(PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.11/12/2023)
……
Na Rahma Khamisi Maelezo. 11/12/2013
Jamii nchini imetakiwa kuilinda na kuitunza lugha ya Kiswahili ili kuhifadhi Utamaduni wa waswahili na Waafrika kwa ujumla.
Akifunga Kongamano la Saba la Kiswahili Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Mhe, Othman Masoud Othman katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul_Wakil Kikwajuni amesema kuendelea kuitunza lugha hiyo ni kuimarisha na kudumisha utamaduni uliopo nchini.
Amesema lugha ni utamaduni na utambulisho wa jamii fulani, iwapo itaachwa ipoteze uasili wake lugha hiyo ni kuupoteza utamaduni ni vyema kuitumia ipasavyo ili iendelee kuwepo katika taifa.
“Tutambue kwamba mtu mwenye kupoteza uasili wa lugha yake sawa na mti uliokauka na kupoteza majani, maua, matawi, matunda na mwishowe mizizi yake ” alifahamisha Makamo.
Mhe. Masoud amefahamisha kuwa mbinu nzuri ya kusambaza Kiswahili ni kuandaa machapisho, vitabu vya lugha na kuifundisha kwa uweledi pamoja na kujenga uhusiano na ushirikiano kwa Mataifa mbalimbali ili kuongeza maarifa na kubadilishana uzoefu.
Ameeleza kuwa mafunzo yanayotolewa na Baraza la Kiswahili kwa kufundisha wageni ndani na nje ya nchi yanaendelea kusaidia kupata walimu wenye uzoefu na utaalamu wa lugha ya Kiswahili yatakayorahisisha kuifundisha kwa umahiri zaidi.
“Umefika wakati sasa kwa Balozi zetu zilizopo nje kuhamasisha usomeshaji wa kiswahili katika Mataifa yanayotuwakilisha”, alisisitiza Mhe Masoud.
Ameongeza kuwa ni wajibu wa Serikali kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mataifa hayo kwani usomeshaji wa lugha hiyo katika nchi za kigeni ni jambo lenye umuhimu wa pekee juu ya uimarishaji wa mawasiliano na kueneza utamaduni.
Ameeleza kuwa lugha ya kiswahili ina utajiri mkubwa wa maneno ya lugha kwa kutumia lahaja hivyo hakuna budi kuzitumia lahaja hizo ili kuitunza zaidi.
“Tujifunze lugha yetu iendelee kuwepo kwani lugha ni utamaduni na inabainisha utamaduni wa watu katika maeneo husika “alisisitiza Makamu Masoud.
Hata hivyo amewasihi wasomi kuweka mkazo wa kufanya tafiti ili kubaini changamoto zilizomo katika lugha hiyo ya kiswahili na kuzipatia ufumbuzi.
Akitaja Maazimio ya Kongamanano hilo Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili (BAKIZA) Dkt.Mwanahija Ali Juma amesema katika kuikuza lugha ya Kiswahili wameazimia kuongeza juhudi ya kuitumia lugha hiyo ili iendelee kutumika na kuenea duniani kote.
Amefahamisha kuongeza juhudi za kutafuta watafsiri wa lugha hiyo kwa kuwasadia wale wasiyoielewa lugha hiyo ili nao waweze kuifahamu kwa urahisi.
Azimio jengine ni kuwahamasisha wanafunzi kusoma lugha hiyo pamoja na mikakati ya kuajiri walimu na kuwapeleka nje ya nchi kufundisha wageni.
Dr. Mwanahija amesema kongamano hilo wamependekeza kwamba nchi zote zinazotumia lugha ya Kiswahili kuziandika nyaraka zao kwa lugha hiyo pamoja na kuweka mikakati maalumu kwa wanafunzi kufahamu na kutumia methali ili zisipotee.
Aidha Katibu Mtendaji amevitaka vyuo vikuu vijikite katika kutafuta wakalimani na watafsiri wa lugha ya Kiswahili ili kuendeleza lugha hiyo pamoja na kufanya utafiti wa kiuchumi ili kupata misamiati mingi ya Kiswahili.
Kongamano hilo la saba limeandaliwa na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.