Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka(Mwenye suti nyeusi kushoto) akiwa pamoja na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Iringa, Dkt. Alfred Mwakalebela (katikati), wakiteta jambo na Prof. Ipyana Mwampagatwa (wa kwanza kulia), mara baada ya kuwasili hospitalini hapo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka (mwenye suti katikati) akiwa na baadhi ya maafisa wakati wa kikao na Mganga Mfawidhi (hayuko pichani) alipowasili kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Makamu Mkuu wa Chuo akiwa na madaktari na wahudumu katika moja wapo ya wodi za wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU), akipata maelezo ya huduma na vifaa vinavyotumika kutoa huduma kwa wagonjwa wanaolazwa kwenye wodi hizo.
Baadhi ya wanafunzi wa Udaktari Mwaka wa Nne kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma wakimsikiliza kwa makini Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka (hayupo pichani) alipofanya mazungumzo nao wakati alipotembea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
.……………………….
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na kufanya mazungumzo na Mganga Mfawidhi Dkt.Alfred Mwakalebela na wanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Udaktari mwaka wa nne, wanaofanya mafunzo kwa vitendo Hospitalini hapo.
Akiwa ameambatana na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Razack Lokina; walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya huduma katika Hospitali hiyo na kukagua vifaa na aina ya mafunzo wanayopata wanafunzi wa Udaktari wanaofanya mafunzo katika hospitali hiyo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali hiyo, Prof. Kusiluka, aliupongeza uongozi wa Hospitali kwa huduma nzuri na vifaa vya kisasa ambavyo vimefungwa na Serikali kwa lengo la kutoa huduma, na kwamba kwa mazingira yalivyo ni dhahiri kwamba wanafunzi wanaopata mafunzo kwa vitendo Hospitalini hapo wanajifunza mambo mengi kama mafunzo ya udaktari yanavyotaka.
Aidha; amewataka wanafunzi wanaoshiriki mafunzo hayo kutumia vizuri muda walionao kujifunza na kuwatumia ipasavyo watumishi wenye ubobevu na mabingwa katika utabibu, ili waweze kunufaika na mafunzo wanayoyapata, ili pindi watakapohitimu mafunzo yao waweze kuwa madaktari bora na wa viwango.
Naye Mganga Mfawishi, Dkt. Alfred Mwakalebela, amemhakikishia Makamu Mkuu wa Chuo ubora katika mafunzo wanayoendelea kuyatoa kwa wanafunzi waliopo hospitalini hapo na kwamba kama msimamizi Mkuu wa Hospitali na mafunzo anahakikisha kwamba kila mwanafunzi anakuwa chini ya uangalizi wa madaktari bingwa na wabovu katika fani ili kujifunza mambo mengi, na kukazia sana suala la nidhamu na maadili ya udaktari wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Makamu Mkuu wa Chuo, Mkuu wa Shule Kuu ya Tiba na Afya ya Kinywa, Prof. Ipyana Mwampagatwa amesema kwa sasa jumla ya wanafunzi 350 wa mwaka wa nne na watano wako kwenye mafunzo kwa vitendo, kati yao 170 wako katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa, na 180 wako katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa UDOM.
Hii ni ziara ya kwanza ya Makamu Mkuu wa Chuo kutembelea na kufanya mazungumzo na wanafunzi wa Shahada ya kwanza ya Udaktari wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.