Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Eugenius Hazinamwisho akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke leo Disemba 7, 2023 Jijini Dar es Salaam, ambapo kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu siku ya Disemba 10, 2023 na Siku ya Uhuru Disemba 9, 2023 katika ofisi za Takukuru Mkoa wa Temeke wanatoa elimu kwa wananchi wote wanaofika katika ofisi hizo pamoja na maeneo mbalimbali.
Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bi. Esther Mkokota (kushoto) akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kuzuia vitendo vya rushwa kwa kila wananchi anaefika katika ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Temeke Jijini Dar es Salaam kupata huduma pamoja na maeneo mbalimbali.
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wananchi pamoja na Watendaji kutoka sekta mbalimbali wametakiwa kuwa wazalendo kwa Taifa kwa kushiriki katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa kufata sheria, kanuni na taratibu katika kutoa haki ikiwemo kuacha tabia kudai rushwa kwa njia yoyote jambo ambalo ni utomvu wa maadili.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo Disemba 7, 2023 katika Ofisi za
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke ambapo kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu siku ya Disemba 10, 2023 na Siku ya Uhuru Disemba 9, 2023 wanatoa elimu kwa watu wote wanaofika katika ofisi hizo pamoja na maeneo mbalimbali ndani ya TAKUKURU Mkoa wa Temeke.
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bw. Eugenius Hazinamwisho, amesema kuwa ni muhimu kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi katika utekelezaji wa majukumu ili kuleta tija kwa Taifa.
Bw. Hazinamwisho amesema kuwa wapo baadhi ya watendaji wanaotumia vyeo na madaraka yao vibaya kwa kudai rushwa kwa njia mbalimbali na kukiuka haki za binadamu kwa kutokutoa maamuzi ya haki, hivyo wakati umefika wa kujitafakari na kuzingatia maadili.
Amesema kuwa serikali inayaongozwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekua ikipeleka fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini baadhi ya fedha zimekua zikiishia katika mifuko ya watu wachache waliokosa maadili na kukwamisha juhudi za serikali
“Ni muhimu kushiriki kwa pamoja kusimamia maadili na kupinga vitendo vya rushwa, tuiunge serikali yetu mkono ili sote tufurahie rasilimali za nchi yetu” amesema Bw. Hazinamwisho.
Naye, Mkuu wa Dawati la Elimu kwaUmma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Bi. Esther Mkokota, ameeleza kuwa usimamizi wa maadili na mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mtanzania, katika kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja jambo ambalo litasaidia matumizi mazuri ya rasilimali za nchi.
Amefafanua kuwa kupitia maadhimisho ya siku ya uhuru pamoja na siku ya maadili na haki za binadamu wakati umefika wa kujitathmini ili kuondokana na vitendo vya rushwa hasa kuzingatia suala la maadili katika nyanja mbalimbali.
Kauli mbiu ya maadhimisho siku ya maadili na haki za binadamu ni “Zingatia Maadili, Utu, Uhuru, na Haki kwa watu wote kwa maendeleo endelevu”