Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akielelzea mafanikio ya OSHA wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa taasisi zilizopo chini ya ofisi ya Msajili wa Hazina kukutana na vyombo vya habari.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akifurahia jambo na Jane Mihanji Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF na Mwajiri kutoka magazeti ya Uhuru na Mzalendo wakati akiwasilisha aalamu za TEF katika kikaokazi hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam Leo.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kosuri akidafanua baadhi ya mambo kabla ya kuanzia kwa kikaokazi hicho.
……………………………
WAKALA wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), umesema kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza maoneo ya kazi yaliyosajiliwa hadi kufikia 30,309.
Mafanikio hayo yameainishwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa taasisi zilizopo chini ya ofisi ya Msajili wa Hazina kukutana na vyombo vya habari.
Mwenda amesema kwa miaka mitatu wameweza kuimarisha shughuli za usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi nchini.
“Katika kipindi tajwa, wakala umefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 30,309, ongezeko hili ni sawa na asimilia 599. Aidha idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia kaguzi 776,968 sawa na asilimia 646,”alisema.
Amesema kaguzi hizo zinahusisha, ukaguzi wa jumla, ukaguzi maalum kama vile ukaguzi wa usalama wa umeme, Vyombo vya Kanieneo, ukaguzi wa vifaa vya kunyanyulia vitu vizito, ukaguzi wa kiegonomia pamoja na tathmini ya vihatarishi vya kimazingira.
Mwenda amesema kumekuwa na ongezeko la asilimia 44.1 ya wafanyakazi waliopata mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia 47,090.
“Mafunzo haya yanajumuisha mafunzo ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na uundwaji wa Kamati za Usalama na Afya, mafunzo ya kufanya kazi katika maeneo ya juu, Mafunzo ya Huduma ya Kwanza, Mafunzo ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali katika maeneo ya kazi, Mafunzo ya Usalama na Afya katika sekta za Mafuta na Gesi pamoja na sekta ya Ujenzi na Majenzi na Mafunzo ya Uendeshaji Salama wa Mitambo,” amesema.
Aidha, amesema kumekuwa na ongezeko la upimaji afya za wafanyakazi kwa asilimia 163 kutoka wafanyakazi 363,820 hadi wafanyakazi 955,959 waliopimwa katika kipindi tajwa.
Amesema ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa wadau wetu, matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kutoa huduma za usalama na afya ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma pamoja na kuimarika kwa uwezo wa taasisi wa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mtendaji huyo amesema mafanikio hayo ya kuongezeka kwa idadi ya maeneo ya kazi na wadau waliowafikia na kuwapa huduma ni kiashiria kwamba hali ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini inazidi kuimarika.
Mwenda amesema pia OSHA imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini yametokana na uongozi wake madhubuti wa Rais Samia yanayoendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala Ibara ya 130 (f) ambapo chama kimewaahidi Watanzania kwamba kitajenga uwezo wa waajiri na wafanyakazi kuhusu afya na usalama mahali pa kazi.
“Wote ni mashahidi na tunaona juhudi ambazo, Rais wetu, amekuwa akizifanya kuhakikisha kuwa wawekezaji wanakuja kuwekeza nchini ikiwemo kuhimiza uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji na hili ni pamoja na maelekezo mbalimbali katika hotuba zake na hata hivi karibuni tumeona katika mabadiliko aliyoyafanya kwenye miundo ya wizara, suala la uwekezaji limepewa kipaumbele na kuhamishiwa katika Ofisi ya Rais,” amesema.
Amesema OSHA itahakikisha uwekezaji nchini unakuwa na tija na manufaa kwa wananchi pamoja na kulinda nguvukazi ya Taifa, ili kuwa na uzalishaji endelevu.
Aidha, amesema katika kusimamia hilo wameweza kufanya maboresho ya kuondoa na kupunguza ada za huduma mbalimbali zaidi ya 15.
“Miongoni mwa maeneo yaliyoonekana kuwa na uhitaji wa maboresho ilikuwa ni kupunguza au kuondoa baadhi ya ada za huduma ambazo zisingeathiri usimamizi na utoaji wa huduma za usalama na afya mahali pa kazi nchini.
OSHA ilipendekeza kuondoa ada ya usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya shilingi 50,000 hadi shilingi milioni 1.8, ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi shilingi 2,000; kufuta faini zinazohusiana na ukosefu wa vifaa vya kuzimia moto ya shilingi 500,000, ada ya leseni ya ithibati iliyokuwa inatozwa shilingi 200,000 kwa mwaka,” amesema.
Mwenda amesema pia wameondoa ada ya ushauri wa kitaalamu wa usalama na afya ya shilingi 450,000, ada ya mafunzo ya elimu kwa umma iliyokuwa inatozwa kiasi cha shilingi 250,000 kwa kila mshiriki; kupunguza ada ya uchunguzi wa ajali iliyokuwa ikitozwa shilingi 500,000 mpaka shilingi 120,000.
Mtendaji huyo amesema wameondoa ada ya kipimo cha mzio iliyokuwa ikitozwa shilingi 25,000 kwa mfanyakazi
kuondoa ada ya kipimo cha kilele cha upumuaji iliyokuwa ikitozwa shilingi 10,000 kwa mfanyakazi.
“Kupunguza ada ya huduma za ukaguzi wa mifumo ya umeme katika vituo vya mafuta vilivyopo vijijini kutoka shilingi 650,000 hadi shilingi 150,000,” amesema.
Amesema punguzo hilo lililenga kuhamasisha uwekezaji katika maeneo hayo, hivyo, kupunguza athari zinazoweza kutokea kutokana na utunzaji wa mafuta kwenye chupa za maji na madumu, suala ambalo linahatarisha maisha ya wananchi katika maeneo hayo.
Mwenda amesema pia wameondoa ada ya ukaguzi wa usimikaji wa pampu za gesi kwa kila kituo ambayo ilikuwa inatozwa shilingi 20,000 kwa kila pampu.
“Ada zilizofutwa ama kupunguzwa na OSHA zimeleta unafuu ambao umechochea ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini ikiwemo kuongeza ajira kwa Watanzania,” amesema.
Mwenda amesema ada zilizofutwa ama kupunguzwa zinakadiriwa kuwa zaidi ya shiling bilioni 35 ambazo Rais ameelekeza fedha hizo zitumike katika kuimarisha mifumo ya kulinda wafanyakazi ili waweze kuzalisha kwa tija.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni
usimikaji na Uboreshaji wa Mifumo ya TEHEMA, Kuimarisha Mifumo ya Usalama na Afya katika Miradi ya Kimkakati, Tanzania kutambulika Kimataifa katika Masuala ya Usalama, Afya Mahali pa Kazi na Ujumuishaji Sekta isiyo rasmi katika Mfumo Rasmi wa Usimamizi wa Maeneo ya Kazi na mengine mengi