Mwenyekiti wa chipukizi wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Iqra Amani Said Kweka ameitaka jamii kuripoti na kuzuia vitendo vya kikatili vinavyofanywa dhidi ya watoto ikiwemo vipigo, unyanyasaji na mimba za utotoni.
Hayo ameyasema wakati wa ziara yake katika viwanja vya shule ya awali na msingi Pendo iliyopo kata ya Kawekamo wilayani Ilemela Kwa lengo la kuhamasisha uhai wa jumuiya hiyo pamoja kuhamasisha jamii kupinga ukatili ambapo ametoa wito kwa wazazi kuruhusu watoto wao kujiunga na chipukizi sanjari na kuwalinda, kuwatia moyo na kuwasaidia ili watimize ndoto zao.
‘.. Niiombe jamii kuvipinga vitendo vya kikatili hasa ndoa za utotoni lakini pia muwaunge mkono watoto katika masomo ili tutengeneze viongozi wa sasa na baadae ..’ Alisema
Aidha Mwenyekiti Iqra amewashukuru wajumbe wa mkutano Mkuu wa chipukizi wilaya ya Ilemela kwa kumuamini na kumchagua kuwa Mwenyekiti wao huku akiahidi kuwatumikia Kwa haki na uadilifu mkubwa.
Kwa upande wake Katibu wa uhamasishaji na chipukizi wilaya ya Ilemela Ndugu Salvatory Samwel mbali na kumsifu Mwenyekiti huyo Kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwatumia chipukizi wa UVCCM wa wilaya hiyo amewataka wazazi kuacha dhana potofu walizonazo zinazopelekea kuwazuia vijana kujihusisha na siasa kwani kufanya hivyo kunalikosesha taifa viongozi wazuri wa baadaye.
Kadogo Marwa Matiku ni Katibu wa CCM kata ya Ibungilo ambapo amempongeza Mwenyekiti huyo Kwa kuchaguliwa lakini pia amemuahidi ushirikiano kuhakikisha jumuiya hiyo na chama vinasonga mbele.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa chipukizi wilaya ya Ilemela alifanikiwa pia kugawa vifaa vya shule kama madftari na kalamu Kwa wanafunzi wa shule ya awali na msingi Pendo kama ishara ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya CCM kwa kuboresha sekta ya elimu nchini.