Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaabani akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusiana na Maandalizi ya Maonesho ya Biashara ambayo yatafanyika Kuanzia Tarehe Saba January na kumalizia Tarehe Tisa katika Eneo maalum Nyamanzi Dimani ambapo kauli mbiu yake ni “Biashara Mtandao ya Maendeleo ya Biashara na Uekezaji”hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Wizara hio Gulioni Jijini Zanzibar.
…..
Khadija Khamis – Maelezo ,05/12/2023
Wizara ya Biashara, Maendeleo ya Viwanda, inatarajia kufanya maonesho ya 10 ya biashara ambayo yatakwenda sambamba na Sherehe za Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akitoa kauli hiyo Waziri wa Wizara hiyo, Omar Said Shaaban, wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali huko katika ukumbi wa Wizara hiyo Gulioni , Unguja,
Amesema lengo la maonesho hayo ni kuwapa fursa wananchi hasa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, kuzitangaza bidhaa zao wanazoingiza, wanazotengeneza na kuuza hapa nchini.
Aidha alisema maonesho hayo yatatoa fursa kwa Taasisi za Serikali kuzitangaza huduma mbali mbali zenye mnasaba wa biashara wanazozifanya kwa wananchi.
Shaaban alisema Serikali ya awamu ya nane imeahidi kutoa eneo la kudumu huko nyamanzi kwa lengo la kuendeleza mradi wa viwanja vya maonesho.
“Ni mradi mkubwa wakudumu na wakisasa ambao serikali imeekeza kwa kiwango kukubwa cha fedha hivyo iko haja ya kuhakikisha mradi huo unasimamiwa vyema ili kufikia malengo yaliyokusudiwa , ” alisema Waziri huyo.
Hata Hivyo aliwataka wafanyabiashara na wajasiriamali wakubwa na wadogo wenye nia ya kuonyesha bidhaa zao pamoja na huduma wanazozitoa kwamba maonyesho yataanza Januari saba na kumalizika kwake Januari 19, 2024.
Wakati huo huo Waziri huyo alizindua nembo itwayo (ZITF) Zanzibar Internetional Trade Fair.
Alisema shughuli zote za matukio yatakazoendelea katika maonyesho hayo zitarushwa moja kwa moja katika mitandao ya kijamii ili wananchi ambao hawakubahatika kufika huko wapate fursa ya kujionea ,
Alisema ujumbe wa mwaka huu “Biashara Mtandao ya Maendeleo ya Biashara na Uwekezaji”