Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji mkuu wa RITA ametoa siku 14 kwa uongozi wa mpito wa msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza kuhakikisha fedha zilizochukuliwa kinyume cha utaratibu kutoka kwa wafanyabiashara waliopanga katika vyumba vinavyozunguka msikiti huo kurejeshwa pamoja na kuandaliwa kwa taarifa ya mapato na matumizi itakayowasilishwa katika ofisi yake.
Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani Mwanza kwaajili ya kusikiliza kero na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara waliopanga katika vyumba vya msikiti huo na viongozi walioondolewa madarakani uliofanyika katika ukumbi wa TANROADS Mwanza, Mkurugenzi mkuu wa RITA na Kabidhi wasii mkuu Bwana Frank Kanyusi amekemea uongozi wa mpito wa msikiti huo kujihusisha na majukumu yaliyo nje ya mipaka yao sanjari na kuacha kupokea fedha za msikiti kinyume na taratibu.
‘.. Natoa siku 14 muwe mmeandaa taarifa iliyokamilika ya mapato na matumizi na namna mnavyotekeleza majukumu yenu, mna wapangaji wangapi, mna mali kiasi gani, na kuhusu malalamiko ya fedha ambayo mmekiri kuzipokea mzirudishe kwenye akaunti ya benki ya Amana inayomilikiwa na msikiti ..’ Alisema.
Aidha Mhe Kanyusi ameutaka uongozi wa baraza kuu la waislam mkoa wa Mwanza BAKWATA kuhakikisha unakamilisha rasimu ya msikitini huo ili uchaguzi kwaajili ya kupata viongozi wapya uweze kufanyika sambamba na kusisitiza kuusimamia vyema ili kuzuia vitendo visivyofaa.
Kwa upande wake Naibu Kabidhi Wasii Mkuu Bi Irene J Lesulie amewaasa viongozi walioondolewa madarakani, waumini na wafanyabiashara waliotoa malalamiko yao dhidi ya uongozi wa mpito kuwa na imani na Serikali na kwamba kero na changamoto zote zilizowasilishwa zitaenda kufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Nae mwakilishi wa baraza kuu la waislam BAKWATA mkoa wa Mwanza Hasan Fatiu amemhakikishia kabidhi wasii mkuu kuwa baraza la waislam mkoa wa Mwanza litakamilisha kwa haraka rasimu ya msikiti huo ili kuweza kupata viongozi wapya ambapo awali ilishindikana kutokana na kesi za mara kwa mara zilizokuwa zikifunguliwa na pande mbili za uongozi wa zamani na mpya wa mpito hivyo kusuasua kwa ukamilishaji wake kwa wakati pamoja na changamoto za kifedha katika kutekeleza majukumu yake.
Bi Magreth Longino ni mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Nyamagana, yeye amekemea usimamizi mbaya wa mali za msikiti ikiwemo gari la msikiti huo pamoja na kuagiza kurejeshwa mara moja msikitini gari hilo ili liweze kuendelea na shughuli zake
Akihitimisha mwenyekiti wa kamati ya mpito ya msikiti wa Ijumaa Shekh Amani Mauba mbali na kukiri baadhi ya malalamiko yaliyotolewa dhidi yake ameahidi kusimamia uwasilishaji wa fedha zote zilizopokelewa kinyume cha utaratibu katika akaunti ya msikiti pamoja na kusimamia uandaaji wa taarifa ya mapato, matumizi na utendaji kazi itakayowasilishwa kwa kabidhi wasii mkuu
Kabidhi wasii mkuu na afisa mtendaji mkuu wa RITA ameahidi kurudi jijini Mwanza mara baada ya siku hizo 14 kwaajili ya kuzungumza tena na wafanyabiashara waliopanga katika vyumba vinavyomilikiwa na msikiti, viongozi walioondolewa madarakani na uongozi wa mpito kwaajili ya mrejesho wa utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa