Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius. W. Kahyarara ametembelea banda la maonesho la TMA katika Mkutano wa 16 wa Wadau wa Sekta ya Uchukuzi kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini (16th JTSR) unaofanyika jijini Arusha, tarehe 05 hadi 08 Desemba 2023 na kuagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza mafanikio ya taasisi yanayopatikana kikanda, kimataifa pamoja na mafanikio yanayopatikana katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi.
Katibu Mkuu pia ameisifu TMA kuwa ni taasisi inayofanya kazi nzuri na yenye mafanikio kitaifa na kimataifa.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa “ni wakati sasa, jamii ikatambua mafanikio ya TMA kikanda na kimataifa, natambua kuwa taasisi hii inafanya kazi nzuri inayoonekana, ni vyema kujipanga kuwa na vipindi katika televisheni na kueleza mafanikio hayo”.Alizungumza Prof. Godius. W. Kahyarara, wakati akitembelea mabanda ya maonesho ya wadau wa sekta ya Uchukuzi.
Aidha, Katibu Mkuu aliitaka Wizara kusimamia program ya kutangaza mafanikio ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi kwa kuanza na TMA.
Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Miundombinu na Ufundi, Dkt. Pascal Waniha, alieleza kuwa TMA imekuwa kielelezo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na nje ya Kanda.
“Kazi kubwa imeendelea kufanyika katika kuiwakilisha nchi vizuri kwenye masuala ya hali ya hewa kimataifa na kueleza kuwa imeteuliwa na WMO kuwa muandaaji wa mafunzo ya rada katika Kanda ya Afrika yanayoratibiwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Fursa hii imepatikana kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Alisema Dkt. Waniha.
Mafanikio mengine yaliyoelezwa mbele ya Katibu Mkuu kupitia mabango ni pamoja na maendeleo katika shughuli za uangazi, ununuzi wa vifaa na mitambo ya hali ya hewa, udhibiti wa huduma za hali ya hewa pamoja na njia mbalimbali zinazotumika katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii na kwa sekta mahsusi.