Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof.Joyce Ndalichako akimkabidhi kikombe Afisa Mkuu Raslimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonnay baada ya Benki hiyo kuibuka washindi wa Pili wa jumla wakati wa sherehe za kutoa Tuzo ya kutambua Mwajiri bora wa mwaka 2023 zilizofanyika jijini Dar es Salaam
Afisa Mkuu Raslimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonnay akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE Bi. Suzanne Ndomba akizungumza wakati wa utoaji wa tuzo hizo uliofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
……………………………..
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka waajiri kutoa ushirikiano kwa Chama cha Waajiri nchini (ATE) kwa kutoa nafasi kwa wahitimu kuja kujifunza kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi.
Ameyasema hayo leo Desemba 4,2023 katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako, wakati wa utoaji tuzo za mwajiri bora wa mwaka zinazoandaliwa na ATE.
“Suala la kukuza ujuzi ni letu sote yaani sekta binafsi na serikali, ushirikiano katika hili utaleta mabadiliko ya haraka katika kutekeleza azma ya kujenga rasilimali watu yenye ujuzi wa stadi mbalimbali,” amesema Majaliwa.
Pia amewataka waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kurahisisha utekelezaji wa malengo ya mifuko hiyo ikiwemo kulipa mafao na malipo ya mfanyakazi anayepata ugonjwa akiwa kazini na ulemavu wa kudumu.
“Ili kuwaondolea wastaafu usumbufu waajiri hakikisheni mnawasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, waliochelewesha michango wahakikishe wanalipa na tozo kwa wakati ili wafanyakazi wanapostaafu wapate stahiki zao katika muda uliopangwa,” amesema.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzzane Ndomba, amesema tangu kuanzishwa kwa tuzo ya mwajiri bora wa mwaka imeendelea kuwa tukio muhimu kwa waajiri wote nchini linalotambulika katika ngazi ya kitaifa na kuhamasisha kampuni wanachama kuweka juhudi katika masuala ya ajira na usimamizi wa rasilimali watu.
Amevitaja vipengele 14 vilivyoshindaniwa kuwa ni ubora katika usimamizi wa rasilimali watu, utofautishwaji na ushirikishwaji, masuala ya utawala na uongozi, ukuzaji wa vipaji, kusaidia jamii, ushirikishwaji wa mwajiriwa na uwajibikaji katika mwenendo wa biashara na utendaji unaokidhi.
Vipengele vingine ni uwajibikaji katika mwenendo wa biashara na utendaji unaokidhi, mafuzo ya ujuzi wa kazi na uanagenzi, maudhui ya ndani, ubora, uzalishaji na ubunifu, mabadiliko ya tabia nchi, namna ambavyo makampuni yanakabiliana na majanga yanayotokea katika maeneo ya kazi, usawa wa kijinsia na usawa katika maeneo ya kazi na kampuni inayofuata miongozo na matakwa ya kisheria.
Katika tuzo hizo Kampuni ya Barrick NorthMara iliibuka mshindi wa jumla wakati Benki ya NMB iliibuka mshindi kwa upande wa sekta ya umma na Kampuni ya Serengeti Breweries ikiibuka mshindi wa pili.