K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
MAHAKAMA
Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, imeeleza utayari kushirikiana na Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wa kufanyia marekebisho baadhi ya sheria zinazohusu
masuala ya fidia, ili kuboresha huduma za fidia kwa walengwa, Jaji Mfawidhi wa
Mahakama hiyo, Mhe, Dkt. Yose Joseph Mlyambina, amesema.
Mhe.
Dkt. Mlyambina, amesema hayo jijini Arusha, kwenye Kikao Kazi baina ya WCF na
Majaji wafawidhi, Majaji wa Kanda, Watendaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi pamoja na Watendaji wa Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi (CMA), jijini Arusha, Disemba 2, 2023.
“Naamini
tutaendelea kuiboresha kwa kina, sheria yetu, kwa manufaa yetu sisi kama
Watanzania, sisi waheshimiwa majaji, waheshimiwa manaibu wasajili na
wasuluhishi wote, tuko tayari kutoa mawazo yetu kutokana na uzoefu tunaoupata
kazini, kwa ajili ya kuboresha sheria yetu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.”
Alifafanua Dkt. Mlyambina.
Amesema,
anatamani WCF iwe mfano wa kuigwa sio tu Barani Afrika bali Duniani kote katika
masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi na kuishukuru
Bodi ya Wadhamini ya WCF, kwa kuisimamia vema taasisi hiyo.
“Hakika
wanatekeleza vema majukumu yao kwa faida ya Watanzania, mtakubaliana nami, elimu tuliyoipata hapa ina mchango mkubwa sana katika
kuiboresha sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, na hii sio tu kwamba ina
manufaa kwa Mfuko, bali kwa Watanzania wote.”Amesema Jaji Mlyambina.
Naye
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocat
Mteule, amesema WCF ina faida kubwa sana kwa wafanyakazi na kwakuwa sheria zinaendelea
kuboreshwa, ana mataumaini makubwa kuwa Wafanyakazi watanufaika zaidi
na Mfuko.
“Rai
yangu mimi leo ni kwa waajiri, kuona umuhimu huo, kwa sababu sio kwa faida ya
mfanyakazi peke yake, inapotokea mfanyakazi ameumia kazini, huo ni mzigo wako
lakini badala ya kubeba mzigo huo, tambua kwamba WCF ipo na jukumu
lake ni kumuhudumia mfanyakzi aliyepatwa na changamoto akiwa kazini.” Amesema,
Mhe. Mteule.
Naye Mkurugenzi
wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Bw. Usekelege Mpulla, amesema, Kikao Kazi
hicho kina manufaa makubwa kwani wote kazi yao ni kuwahudumia waajiri na waajiriwa.
“Yapo
baadhi ya mashauri yanakuja kwenye Tume, lakini kwa yale mashauri ya kuumia kazini, yanaweza kuhudumiwa na WCF, hivyo CMA inabadilishana taarifa na WCF na hivyo kuwawezesha wananchi kuhudumiwa kwa wakati.” Alifafanua.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, aliwashukuru Waheshimiwa
Majaji Wafawidhi na washiriki wote kwa kuhudhuria.i“Bilashaka mmepata picha halisi ya namna WCF iunavyofanya kazi, na kwa kwa upande wetu tumepata nafasi
nzuri ya kujifunza mengi kutoka kwenu na tunawaahidi kuendeleza ushirikiano na Mahakama.
“Mimi
kwa niaba ya Manejiment na Bodi ya Wadhamini, tunaahidi kuyachukua mapendekezo
mliyoyatoa ili kuboresha sheria yetu.” Alibainisha.
Amesema
WCF imeanza kuyafanyia kazi mapendekezo ya Waheshimiwa Majaji, kuhusu sheria
mbalimbali zinazohusu fidia kwa wafanyakazi.
Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter, akitoa mada
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini, WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar, akitoa mada.
Dkt. Mduma, akipeana mikono na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga, huku Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (katikati) akishuhudia.
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji na washiriki wengine .