Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Amani Abeid Karume amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwenda kuwatumikia wananchi kwa weledi na upendo huku wakiendelea kujiendeleza zaidi na elimu.
Wito huo ameutoa leo Desemba 2,2023 jijini Dar es salaam kwenye mahafali ya 17 ya Chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi muhimbili MUHAS.
Amesema wanapaswa kujitolea kufanyakazi kwa upendo ili kuhakikisha wanaisaidia jamii na taifa kwa ujumla ili kuendelea kuleta maendeleo endelevu katika taifa.
“Niwaambie huu sio mwisho leo mnatunikiwa muende mkaisaidie jamii yenu kwa upendo kwani upendo ndio maendeleo ya elimu katika taifa hivyo wengine muendelee kujiendeleza kielemu zaidi”amesema Karume.
Kwa upande wake Makamu mkuu wa chuo Profesa Aporinary Kamuhabwa amesema wataendelea kutoa elimu kuendena na teknolojia pia kufanya tafiti ambazo zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya afya.
Aidha Profesa Kamuhabwa ameipongeza serikali kwa kuongeza rasilimali watu katika chuo hicho ambapo takribani wanataaluma 111 na wasaidizi wa taaluma 11 wameajiliwa chuoni hapo.
“Tutaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha idadi ya watumishi inaongezeka kulingana na uhitaji unaohitajika lakini pia chuo kimeshirikiana na serikali kuboresha miundombinu ya chuo lakini kuendelea kushirikiana ili tufanikishe ujenzi wa chuo kipya Kigoma”amesema Kamuhabwa.
Nae,mwakilishi wa wahitimu wa shahada za awali Whitefrank Frank,ambae ni muhitimu wa shahada ya udaktari wa kinywa na meno amesema ni wajibu wao kubeba majukumu waliyopewa kwa nidhamu,weredi na upendo kwani wameichagua fani ya afya wao hivyo awanabudi kuitumikia.
Hata hivyo,Mwakilishi wa wahitimu wa shahada za uzamili Merciana Mliga amepongeza jitihada za Rais dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya afya kwa kuweka mazingira wezeshi ya ufanyajikazi lakini ufadhiri wa masomo kwa ngazi mbalimbali.
“Shukrani za pekee ziende kwa serikali ya jamuhuri ya muungano inayoongozwa na mama yetu Dkt Samia Suluhu Hassan amejitoa kwa nguvu zote katika kuboresha sekta ya Afya na elimu kwa kuweka miundombinu wezeshi ya kujifunzia na kufanyia kazi”amesema Mliga.
Mahafali ya MUHAS mwaka 2023 jumla ya wahitimu 1,306 wamehitimu ambapo kati yao 422 ni wahitimu wakike ambao sawa na asilimia 32.3 ya wahitimu wote.