Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolfu Mkenda amesema Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi kinara kwa kudhibiti mianya ya uvujaji wa mitihani.
Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 30,2023 Dar es Salaam wakati akifungua maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA) yaliyobebwa na kauli mbiu isemayo ‘Upimaji wa umahiri kwa misingi ya haki suluhisho la ajira karne ya 21’.
Mkenda amesema pamoja na kuwepo na changamoto mbalimbali za wizi wa mitihani lakini Tanzania ipo vizuri kudhibiti mianya hiyo kuliko nchi nyingine.
“Ninalipongeza Baraza la Mitihani Tanzania kwa kampeni mliyoianzisha ya kuzuia wizi wa mitihani, mbali na changamoto iliyopo bado Tanzania tupo vizuri kudhibiti wizi wa mitihani ukilinganisha na nchi nyingine,”amesema.
Profesa Mkenda amesema mtu akishiriki katika wizi wa mitihani anakuwa anaharibu maadili ya mtoto hivyo ameshauri walimu wakiwashindanisha wanafunzi wao wahakikishe hawahusiki na wizi huo.
“Huwa nasikitika kusikia wizi wa mitihani ukihusisha walimu na baadhi ya viongozi nawaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na kamati za mitihani mnaposhindanisha shule mtumie miongozo iliyowekwea na msishindanishe kwa kuhamasisha wizi wa mitihani,” amesema.
Profesa Mkenda amesema wizara inatarajia kufanya kampeni nchi nzima kuhamasisha mtoto kujilinda zaidi kwa lengo la kuondokana na wimbi la wanafunzi kupata mimba shuleni na kushindwa kutimiza malengo yao.
“Tunasikitika kuona idadi ya wanafunzi wanaojiandikisha darasa la kwanza sio wanaohitimu darasa la saba hivyo tutafanya utafiti na kubaini mikoa ambayo ni tatizo kwa sababu hatuwezi kuvumilia wale waliojiandikisha darasa la kwanza hawamalizi shule,” amesema.
Pia amewataka walimu na watendaji kuhakikisha michango wanayoichangisha shuleni isiwe kikwazo cha wanafunzi kushindwa kwenda shule ndio maana serikali imefuta ada.
Naye Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed amesema wamejipanga kikamilifu kutekeleza mabadiliko ya sera ya elimu na mitaala mipya.
Amesema NECTA inatarajia kufanya upimaji utakao weza kubaini uwezo wa kufikiri na kutenda ambao utaendana na mabadiliko ya sera.
Akizungumzia miaka 50 amesema mafanikio yaliyopo yamewezekana kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi nchini.
“Katika kuadhimisho miaka 50 tulifanya kongamano la Kitaaluma katika chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA)lakini kwa kutambua sisi NECTA ni watumizi wakubwa wa karatasi hivyo tuliendesha zoezi la kupanda miti” amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba ameahidi kushirikiana na NECTA katika kudhibiti vitendo vya udanganyifu wa mitihani vinavyotendwa na baadhi ya watu.