Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Bernard Mayemba akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 29, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati wa zoezi la kuwaondoa wadaiwa sugu katika Nyumba za Mbezi Beach.
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Dar es Salaam umeanza zoezi la kuwaondoa wapangaji sugu ambao hawalipi kodi kwa wakati na katika nyumba za Mbezi Beach na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1.
Akizungumza na wandishi wa habari leo Novemba 29,2023 jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Bernard Mayemba, amesema kuwa nyumba hizo asilimia kubwa wanaishi watumishi wa serikali na wamekuwa hawalipi kodi.
Mhandisi Mayemba amesema kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam kuna nyumba 1,200 hivyo katika zoezi la kuwaondoa wapangaji hawataangalia cheo au sura mtu katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Utaratibu wa huu kuwandoa wadaiwa sugu wa kodi ya pango unaongozwa na dalali ya makahama ni Twins Auction Mart, kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wapangaji wetu kutolipa kodi ya pango kwa muda mrefu” Mhandisi Mayemba.
Amesema kuwa kumekuwa na malimbikizo makubwa ya madeni ya wapangaji huku wengi wakiamini ni nyumba za Serikali hivyo hataweza kutolewa.
Mayemba amesema TBA imeazima kuwafikisha Mahakamani wadaiwa wote lengo likiwa ni kuhakikisha wanalipa madeni yao yote.
“Wadaiwa hao wenye madeni makubwa, wameifanya TBA kushindwa kutekeleza mipango ya ukarabati wa nyumba zilizopo na kujenga nyumba mpya zitakazopangishwa au kuuzwa kwa watumishi wa umma na wananchi wanaokabiliwa na changamoto ya makazi” amesema Mhandisi Mayemba.
Amesema kuwa TBA imefanya maboresho kupitia mfumo mpya wa kielektroniki wa Usimamizi wa Miliki za Serikali (GRMS) ambapo mfumo huo utakuwa unatoza riba ya 20% kwa mpangaji atakae kaa zaidi ya miezi mitatu bila kulipa kodi ya pango.
Zoezi ya kuwaondoa wadaiwa sugu katika Mkoa wa Dar es Salaam litadumu kwa muda wiki tatu ambapo litafanyika katika nyumba na majengo yote yanayosimamiwa na TBA.
Hivi karibuni WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) ilitangaza kufanya kazi na dalali wa mahakama ambaye ni Twins Auction Mart na kukabidhiwa orodha ya wadaiwa wote kwa hatua zinazofuata na zoezi hili litafanyika kuanzia Desemba 1, 2023 katika Mikoa yote nchini.
TBA imesema kuwa hadi sasa jumla ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 7.8 zinadaiwa kwa wapangaji wake zikiwemo taasisi za umma zinazotumia nyumba na majengo yake.
TBA imeazimia kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wapangaji wote tunaowadai, moja ya hatua zitakazochukuliwa ni kuwaondoa wadaiwa sugu kwa nguvu kwa kutumia dalali wa Mahakama ambaye amepewa zabuni hiyo kufanya kazi kwa niaba ya TBA.