Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mwindi kata ya Mbawala wakichota maji.
Mtwara
WIZARA ya maji imefanikisha kuwaondolea kero ya muda mrefu wanafunzi wa shule ya sekondari Mbawala kata ya Mbawala Halmashauri ya wilaya Mtwara ya kubeba ndoo za maji kutoka nyumbani na kupeleka shuleni kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Ni baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji ya bomba wa Mwindi-Ngorongoro uliogharimu jumla ya Sh.milioni 806.
Mwanafunzi wa shule ya sekondari Mbawala Aisha Waziri,ameishukuru serikali kuwajengea mradi huo uliomaliza mateso ya miaka minne kubeba ndoo za maji kichwani kila siku kutoka nyumbani na kupeleka shule na wakati mwingine kwenda mtoni kuchota maji.
Alisema,hali hiyo iliwaathiri sana kitaaluma kwa sababu muda waliotakiwa kuwepo darasani kuanza masomo waliutumia kwenda kuchota maji yanayopatikana mbali na eneo la shule hivyo kuchelewa vipindi darasani.
Alisema baada ya kupata mradi wa maji ya bomba, sasa wanawahi vipindi darasani,kupata chakula kwa wakati kufanya usafi wa mwili,nguo na mazingira ya shule na kuishukuru serikali kwa kuwajengea kituo cha kuchotea maji.
Mwanafunzi mwingine Latibu Said alisema,kabla ya mradi huo hawakuwa na furaha hata kidogo kila wanapofika shuleni kutokana na kukosa huduma muhimu ya maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo usafi wa vyoo ambako ni sehemu muhimu na lazima kwa kila binadamu.
Alieleza kuwa,matumizi ya maji ya visima ambayo hayakuwa safi na salama yalisababisha baadhi ya wanafunzi kuugua magonjwa ya mara kwa mara hasa ya matumbo na kuharisha.
Alisema,baada ya kukamilika kwa mradi huo wanafunzi wana furaha kubwa kwani umemaliza maumivu na mateso makubwa ya kubeba ndoo za maji kichwani na hata kupunguza maambukizi ya magonjwa hayo.
Mkuu wa shule hiyo Anitha Peter alisema,mradi huo umewasaidia katika kitaaluma kwa kuwa sasa wanafunzi wanapata muda mwingi wa kuhudhuria vipindi darasani.
Aidha alisema,mradi wa maji umepunguza tatizo sugu la utoro kwa baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa wanajificha vichakani kabla ya kuingia darasani ili kukwepa kwenda mtoni kuchota maji.
Mwalimu Peter alisema,watatumia maji hayo kufanya vizuri kitaaluma hasa ikizingatia kuwa kwa mara ya kwanza watatoa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka huu,na kuwapongeza wataalam wa Ruwasa waliosimamia na kutekeleza mradi huo.
Kwa upande wake kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Mtwara Mhandisi Abdulaaziz Hemed alisema,mradi wa maji Mwindi-Ngorongoro ulianza kutekelezwa mwezi Machi mwaka 2022 na kukamilika mwezi Machi 2023 kwa gharama ya Sh. 806 na unahudumia watu zaidi ya 6,840 wa vijiji vitatu vya Malongo,Mbawala na Mwindi.
Kwa mujibu wa Hemed ni kwamba,miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mradi ni shule ya sekondari Mbawala ambayo imepata kituo kimoja cha kuchotea maji kichowasaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kwenda shule na ndoo za maji kichwani na kuchelewa kuhudhiria vipindi darasani.
Alitaja kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa tenki la ujazo wa lita 100,000,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 16,tenki la chini la ujazo wa lita 100,000 na ukarabati wa matenki mawili ya ujazo wa lita 50,000 kila moja katika kijiji cha Malongo.