Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu akizungumza leo Novemba 28, 2023 Jijini Dar es Salaam na wahariri wa vyombo vya habari.
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu (kulia) akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw. Deogratius Balile leo Novemba 28, 2023 Jijini Dar es Salama katika Mkutano na Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari.
Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika Mkutano na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu uliofanyika leo Novemba 28, Jijini Dar es Salaam.
………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji wa shilingi trillioni 73 katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala wa Serikali 298 ambazo zinafanya shughuli mbalimbali, huku asilimia 86 za taasisi hizo zikitoa huduma za kijamii.
Imeelezwa kuwa kutokana na mipango na mikakati iliyopo baada ya miaka mitano baadhi mashariki yanakwenda kufanya vizuri, huku watendaji wa mashirika hayo watapimwa kutokana ufanisi wa kazi katika kuhakikisha wanafikia malengo.
Akizungumza leo Novemba 28, 2023 Jijini Dar es Salaam na wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amesema kuwa kutokana uwekezaji huo kwa mwaka wa fedha 2022/23 mashirika 108 yameweza kupata mapato ya shilingi bilioni 777.
Bw. Mchechu amesema kuwa kwa mwaka 2021/2022 mashirika 136 yameweza kupata mapato ya shilingi bilioni 645 na mwaka 2020/2021 mashirika 200 yamepata bilioni 477, huku mwaka 2019/2020 mashirika 236 yameingiza mapato ya bilioni 696.
“Lengo ni kuhakikisha mashirika ya umma yanafanya kazi kwa ufanisi na kuleta faida kwa serikali katika kuhakikisha yanasonga mbele” amesema Bw. Mchechu.
Bw. Mchechu amesema kuwa wakati umefika kwa wakurugenzi wa mashirika ya umma kufanya kazi wa uweledi katika kuhakikisha wanapata mafanikio katika utendaji wao.
“Ili mashirika ya umma yapige hatua yanapaswa kutoingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake, kuwekeza rasilimali fedha katika kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwekeana malengo na wasimamizi katika kufikia viwango vya mafanikio ndani ya muda fulani” amesema Bw. Mchechu.
Amesema kuwa mipango iliyopo kutakuwa na utaratibu wa kuishirikisha Mamlaka kwenye mchakato wa kuwapata wenyeviti, wajumbe wa Bodi na watendaji wakuu wa taasisi jambo ambalo itasaidia katika ufanisi wa kazi.
Bw. Mchechu amesema kuwa taasisi za umma zinapaswa kuwekewa mifumo rafiki ambayo itasaidia kutengeneza mapato na kuleta tija kwa Taifa.
Bw. Mchechu amesema kuwa ili kufikia malengo wamependekeza mambo muhimu ya kuzingatia ikiwemo kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (PIA) kwa kubadilisha jina la ofisi ya Msajili kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority- PIA) ili kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa duniani.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa
mfuko wa serikali kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati itasaidia kuongeza ufanisi wa uendeshaji, kuokoa mashiriki ambayo bila mfuko huo yanaweza kuanguka pamoja na kuwezesha mashirika ya umma kustahimili ushindani.
“Kuainisha vyanzo vya fedha za mfuko wa uwekezaji wa umma ambapo vyanzo vya fedha za mfuko vitakuwa ni pamoja na sehemu ya maduhuli yatakayokusanya na mamlaka ambayo kiwango chake kitabainishwa kwenye kanuni” amesema Bw. Bw. Mchechu.
Nae Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw. Deogratius Balile, ametoa pongezi kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuwafanya kazi kwa ufanisi huku akieleza kuwa vyombo vya habari vitaendelea kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali ya maendeleo.