Na Mwandishi wetu, Handeni Tanga.
Makatibu wakuu wa wizara za kisekta leo ijumaa ya tarehe 24.11.2023 wametembelea kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga kujionea hatua mbalimbali za ujenzi wa miundombinu kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya kuhamisha wananchi wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari.
Wakiongozwa na katibu mkuu ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia sera, Bunge na uratibu Dkt Jim Yonaz makatibu wakuu hao wamekagua ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali ikiwemo maji, umeme, madaraja,barabara, shule, Nyumba za makazi na uboreshaji wa huduma za mawasiliano.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo mkuu wa wilaya ya Handeni mheshimiwa Albert Msando amesema vikosi kutoka SUMA JKT vinaendelea na kazi hiyo licha ya kuwepo kwa mvua nyingi.
Ameongeza kuwa awamu ya pili ya ujenzi huo pamoja na miundombinu mingine unahusisha nyumba 5,000 ambapo Nyumba 2500 ambapo zimefikia katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Kwa upande wake Dkt Yonaz amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kushirikiana kwa karibu na watendaji mbalimbali katika kusimamia zoezi la ujenzi wa miundo mbinu.
Dkt Yonaz amesema serikali imejipanga katika kuhakikisha kuwa wizara zote za kisekta zinashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha wananchi wanaoendelea kujiandikisha kuhamia katika nyumba hizo.
Serikali inaendelea na zoezi la kuandikisha wanaonchi wanaohama kwa hiari katika hifadhi ya Ngorongoro na kuwapeleka katika maeneo mengine ili kulinda hifadhi na kuimarisha maisha ya wananchi nje ya eneo hilo.