Afisa biashara na mikopo Kanda ya ziwa kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Janneth Urio akitoa elimu kwa vijana juu ya namna ya kuwajengea uwezo wa kubadilisha Kilimo kuwa ajira.
Vijana kutoka vikundi mbalimbali vya ufugaji,kilimo pamoja na uchakataji wa vyakula vya mifugo wakiwa kwenye mafunzo
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana 50 Jijini Mwanza juu ya kubadilisha Kilimo kuwa ajira ili waweze kujiinua kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Afisa Maendeleo ya Biashara mwandamizi kutoka (TADB) Angelina Nyasambo, alisema Benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wakulima,wavuvi na wafugaji ambapo kwa kipindi hiki wamefanya na vijana ambao wako kwenye vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na ufugaji, kilimo pamoja na wachakataji wa vyakula vya mifugo.
Alisema kunachangamoto walioiona kwa vijana kutokuwa na maarifa na ufahamu wa Benki ya TADB juu ya utendaji kazi wake ndio maana wakatoa mafunzo hayo ili waweze kuwa na elimu ya kilimo biashara na elimu ya fedha itakayowasaidia kukuza biashara zao.
“Baadhi ya vijana hawafamu kazi zinazofanywa na Benki ya Maendeleo ya kilimo na wengine wanashindwa kuifikia ndio maana tumeamua tukutane nao ili tuwaelimishe kazi zinazofanywa na taasisi yetu pamoja na kuwapa elimu ya kukuza biashara zao”, Alisema Nyasambo.
Alisema mafunzo hayo ni endelevu kwani wamekuwa wakifanya katika Mikoa tofauti tofauti abapi hadi sasa wameshawafikia wakulima, wafugaji na wavuvi zaidi ya 2000.
Alieleza kuwa Baada ya mafunzo huwa tunafuatilia ili kuona kile ambacho tumewafundisha na kuwaelekeza wameweza kukifanyia kazi kwenye biashara zao.
Kwaupande wake Afisa biashara na mikopo TADB Kanda ya ziwa Janneth Urio, alisema Sekta ya Kilimo inakuwa kwa kasi na ni sekta ambayo inafursa nyingi kwa vijana, wanawake na walemavu.
Alisema mbali na kuwajengea uwezo wa kubadilisha kilimo kuwa ajira pia wanawajengea uwezo kwenye Sekta ya uhifadhi ambapo Benki hiyo imekuwa ikiwahimiza kwaajili ya kutimiza sera yake ya kuwa na uhakika wa chakula nchini hatua inayosaidia kupunguza njaa na upotevu wa mazao.
“kuwawezesha vijana na kuwajengea uwezo ni jambo zuri hususani kwenye Sekta ya Kilimo ambayo ni uti wa mgongo na inafursa kubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu vijana wanaweza kuwekeza kwenye kilimo na kukigeuza kuwa kilimo biashara ambacho kinaweza kumpatia ajira na fedha na wakaboresha maisha yao”, Alisema Urio.
Nao baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo kutoka katika kikundi cha Wanamaendeleo kilichopo Kangae Mkoani Mwanza Rafidh Adam na Leila Peter, walisema mafunzo hayo yatawasaidia kubadilisha biashara zao za ufugaji kwa kuzifanya kwa weledi mkubwa kutokana na mbinu mbalimbali walizopewa ikiwemo kuanza kutafuta masoko kabla ya kuanzisha ufugaji.