Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Daniel Godfrey Chongolo amesema kupitia utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi ya 2020 – 2025, CCM itahakikisha Serikali inaendelea kuweka mazingira bora na kuwajengea uwezo makandarasi na washauri waelekezi wazawa, ili waweze kutekeleza miradi mingi na mikubwa ndani ya nchi na hata kushindana nje ya Tanzania, ikiwemo kulipwa madeni yao na kuwahishiwa malipo ya kazi katika miradi wanayotekeleza.
Ndugu Chongolo amesema hatua ya kuwatumia wakandarasi na washauri waelekezi wazalendo wa Kitanzania katika miradi hiyo mbalimbali ya ujenzi itaokoa fedha nyingi, ambazo kwa sasa zinalipwa kwa makandarasi wa nje, hivyo zitabakia katika mzunguko wa fedha na uchumi ndani ya nchi, zitaongeza kipato kwa wahusika, huku pia wakipata nafasi ya kuongeza ujuzi na kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania.
Mbali ya kuwataka watendaji wa Serikali, hususan katika Wizara ya Ujenzi kuacha mitazamo hasi dhidi ya wakandarasi na wahandisi wazawa kuwa hawawezi kazi, pia amewataka baadhi ya makandarasi wa ndani nao kuacha kuichafua tasnia ya ujenzi, kwa kuwa na kampuni za mfukoni (briefcase company), ambazo hazina uwezo wa kufanya kazi, hali ambayo inajenga na kuhalalisha dhana kuwa kuna wazawa wanafanya utapeli kwa kutumia taaluma hiyo.
Katibu Mkuu Ndugu Chongolo amesema hayo leo Jumanne, Novemba 21, 2023, wakati akitoa salaam za Chama Cha Mapinduzi kwenye Mkutano wa Makandarasi na Washauri Waelekezi Wazawa, uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention, jijini Dodoma, ambapo amewaambia kuwa CCM inatambua changamoto zote zinazowasibu, likiwemo suala la madeni wanayodai na kucheleweshewa malipo yao katika miradi anuai wanayotekeleza maeneo mbalimbali nchini.
“Mkutano huu ni muhimu sana. Jana nimekaa na mawaziri wote wawili hawa, Waziri wa Ujenzi na Waziri wa Fedha hadi usiku wa manane, ilibidi tukae kwa muda mrefu sana. Nilitaka kwanza kujua masuala kadhaa kabla sijaja hapa leo. Na hasa nililowaita na kuzungumza nao ni kuhusu malipo yenu. Nina uhakika hapa tukisema tupitishe karatasi kila mtu aandike changamoto yake, jambo la kwanza kila mmoja litakuwa ni malipo, malipo, malipo.
“Wamenieleza kwa kina jinsi wanavyochukua hatua kadhaa, hasa kutekeleza maelekezo na maagizo ya Mhe. Rais Dokta Samia Suluhu Hassan amewaagiza kuhakikisha wanafanya msawazo wa malipo ya madeni ya wakandarasi na pia kila mkandarasi alipwe anapo-raise certificate. Pia labda niseme hapa, ni muhimu mkaenda pia kujifunza kwa wenzenu wa REA (Wakala wa Umeme Vijijini) ili utaratibu ule wanaotumia kulipa wakandarasi wa umeme, uweze kutumika pia huku Ujenzi. Kule hakuna malalamiko sana,” amesema Katibu Mkuu Chongolo.
Pamoja na kuipongeza Serikali kwa kufanya mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi, iliyopandisha kiwango cha thamani ya miradi inayoweza kutekelezwa na wakandarasi wa ndani, kutoka mradi wa thamani ya Tsh. 10 bilioni, hadi kufikia mradi wa Tsh. 50 bilioni, Katibu Mkuu Ndugu Chongolo ameitaka Serikali, kupitia Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Fedha, kuweka utaratibu wa kisheria ambao utakaolazimu ushirikishwaji wa makandarasi wazawa katika miradi yote mikubwa nchini.
“Hili la ushirikishwaji kwenye miradi mikubwa ya kimkakati kama SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, hili tunaweza kulimaliza kwa kuweka sheria ya kulazimisha wakandarasi wakubwa wanapoomba miradi hapa kwetu basi waje na wakandarasi wa ndani kama ilivyo kwa Washauri Majenzi yaani consultants. Hii pia ni nzuri kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
“Mfano tunafanya mradi mkubwa wa SGR lakini mkandarasi akimaliza akiondoka siku tukitaka kufanya ‘ka extension kadogo hata ka kilometa moja, hatutaweza kwa sababu hatukuweka wakandarasi wetu wapate ujuzi. Ni kupitia watu wetu kushiriki, ndiyo tungeweza kufanya kama ambavyo baadhi ya nchi zingine duniani zinafanya kujenga uwezo kwa watu wao kwa kitu kinachoitwa ‘Technological Transfer’,” amesema Katibu Mkuu Chongolo.
Ndugu Chongolo amewahakikishia Makandarasi na Washauri Waelekezi hao wa ndani kuwa CCM itasimamia maslahi yao, kwa kadri ambavyo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025 ilivyoahidi kuwa Chama kitaielekeza Serikali kuhakikisha inaweka mazingira rafiki na bora, ikiwa ni pamoja na kujengewa uwezo wa kupata kazi nyingi zaidi za fedha za Mfuko wa Barabara na kuwawazesha kupata mikopo ili washiriki kikamilifu kwenye miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, madaraja, majengo, maji na mingine mingi.
Katibu Mkuu Chongolo pia aliwataka wazawa hao kutanguliza mbele weledi, uaminifu, kujali rasilimali watu na thamani ya fedha wanapofanikiwa kupata miradi hiyo ya Serikali inayotumia fedha za umma, huku akitoa wito kuwataka waache ubinafsi wa kila mtu kupambana mmoja mmoja katika kutafuta miradi, badala yake watambue umuhimu wa kuungana (Joint Ventures), na wafanye hivyo mapema, si wakati wa kutafuta miradi pekee, ili kujenga kuaminiana katika ubia wa kibiashara wanaokuwa wameingia.