Na John Walter-Manyara
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dr Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka mitatu imetoa shilingi Bilioni 56 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini mkoani Manyara ambapo miradi 64 imekamilishwa na kuzalisha skimu 347.
Hayo yameelezwa na mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maji kwenye vijiji ndani ya Halmashauri sita yenye gharama ya shilingi Bilioni 9,685,375,945.51.
Kupitia Miradi hiyo sita wananchi wapatao 83,624 wanatarajiwa kunufaika kupitia vituo 140 vitakavyojengwa.
Aidha Sendiga amewataka Wakandarasi kufanya kazi kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba kwa muda na ubora.
Meneja wa RUWASA mkoa wa Manyara Mhandisi Walter Kirita ameitaja miradi hiyo iliyosainiwa ni Gijedaboshka wilaya ya Babati, Gunyoda Wilaya Mbulu, Endamaghay wilaya ya Babati ,Madunga wilaya ya Babati , Muguchi wilaya ya Hanang pamoja na Naberera wilaya ya Simanjiro.
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Peter Toima amesema chama kitaendelea kuisimamia serikali kupeleka huduma za kijamii katika maeneo yote.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya za mkoa wa Manyara, Mkuu wa wilaya ya Mbulu Kheri James amesema maji sio anasa bali ni huduma hivyo lazima iwafikie Wananchi wote kama serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inavyosisitiza maji kila kijiji ili kimtua mama ndoo kichwani.
Naye Mhandisi Jumanne Werema kwa niaba ya wakandasi wengine, wameahidi kutekeleza miradi hiyo kwa mujibu wa mikataba.
Amesema amefanya kazi ya Uhandisi kwa miaka 27 lakini RUWASA kwa mkoa wa Manyara ni sehemu pekee ambayo wana utaratibu mzuri unaowawezesha wakandarasi kufanya kazi kwa kuwa ushirikiano.