Na Georgina Misama – MAELEZO
Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Mathew Kundo amesema Serikali ya Tanzania inawekeza fedha nyingi kwenye miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR) hivyo ni wakati sasa vijana kujiandaa kulinda rasilimali hizo kupitia mifumo maalum ya kidijitali.
Mhe. Kundo ameongea hayo leo Novemba 18, 2023 wakati akufungua Majadiliano ya Kitaifa ya Vijana yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yenye lengo la kutoa uelewa zaidi wa matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari kwa vijana hususan wanafunzi wa chuo hicho.
“Mhe Rais, Samia Suluhu Hassan anaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya Kitaifa na kimkakati vijana tujipange kuhakikisha lazima tunatumia mifumo ya TEHAMA kuilinda miradi hiyo, tutangulize uzalendo, vijana jueni ya kwamba nchi yetu inawategemea nyinyi kuhakikisha anga letu la mawasiliano lipo salama,” alisema Mhe. Kundo.
Kwa upande wake Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO Tanzania Michel Toto alisema ni muhimu vijana wajielimishe na kuwaelimisha wengine namna nzuri ya kutumia mitandao ikiwemo kulinda unyanyasaji wa kwenye mitandao hususan kwa wanawake na watoto wa kike kwani ni jukumu la wote.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Lughano Kusiluka alisema katika zama hizi, vijana hawatakiwi kupungukiwa maarifa kutokana na uwepo wa matumizi ya mitandao ikiwa wataitumia kwa usahihi na kwamba matumizi mabaya ya mitandao yana hasara nyingi kwa watumiaji na jamii kwa ujumla.
“Tumefurahi kupata ushirikiano wa Serikali na UNESCO katika masuala TEHAMA tungependa tuendelee kushirikiana zaidi siku za usoni, nataka niwaambie vijana tumieni vizuri nafasi hii jifunzeni na chukueni ushauri wa wataalam, msijisahau fanyeni mambo ambayo yatawafanya muwe watanzania bora,”alisema Prof. Kusilika.