Wizara imepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa inayothibitisha kifo cha Bw. Clemence Felix Mtenga, Kijana Mtanzania ambaye ni miongoni mwa Watanzania wawili ambao pamoja na raia wa mataifa mengine walikuwa hawajulikani walipo tangu yaliyopotokea mapigano tarehe 07 Oktoba 2023, nchini Israel na katika maeneo ya Wapalestina hususan Gaza.
Marehemu Clemence alikuwa ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wapatao 260 waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya Mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.
Tayari Wizara imechukua hatua stahiki ikiwemo kuijulisha familia na inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Israel kuhakikisha kwamba taratibu za kuurejesha mwili wa Marehemu nchini kwa ajili ya mazishi zinakamilika kwa wakati.
Aidha, Wizara inaendelea kufuatilia taarifa za Mtanzania mwingine Ndugu Joshua Mollel ambaye bado hajulikani alipo tangu yalipotokea mashambulizi hayo.
Wizara inatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa msiba huu.
Vilevile, Wizara inapenda kuuhakikishia umma pamoja na Diaspora wa Kitanzania ikiwemo wanafunzi waliopo masomoni nchini Israel kuwa, Serikali kupitia Ubalozi wake uliopo Tel Aviv, Israel, itaendelea kuwasiliana na Mamlaka za Israel ili kuhakikisha Watanzania wote waliopo nchini humo wanakuwa salama wakati wote.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali