Na Sophia Kingimali
Mkurugenzi wa Ifakara Health Institute (IHI) Dkt. Honorati Masanja ametoa rai kwa serikali kuongeza idadi ya watumishi wa afya idara ya mama na mtoto ili kukabiliana na vifo vya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu ili kufikia malengo yaliyoweka.
Wito huo ameutoa leo Novemba 17,2023 jijini Dar es salaam kwenye mkutano wa pili wa kisayansi kuhusu afya ya uzazi mama na mtoto na ikiwa ni maadhimisho ya siku ya mtoto aliezaliwa na uzito pungufu (njiti) duniani.
Amesema watumishi wa afya wanatakiwa kuongezeka ili kufikia malengo yaliyowekwa ya 2030 kuwa na vifo 12 kwa kila vizazi hai 100.000.
“Watumishi wa afya idara ya mama na mtoto wanatakiwa kuongezwa ili waweze kutoa huduma stahiki waliokuwepo ni wachache hawatoshi”amesema Dkt. Masanja
Amesema chumba kinacholaza watoto 50 mpaka 70 kinahitaji manesi wengi tena wenye mafunzo ya kuhudumia watoto wachanga na wanatakiwa wapatikane kwa saa 24.
Amesema mpango wa kuongeza watumishi umetokana na mapendekezo ya utafiti wa kisayansi utaongeza chachu ya kufikia malengo yaliyowekwa.
Kwa upande wake mkurugenzi msaidizi idara ya watoto wachanga na vijana wizara ya Afya Dkt. Felix Bundala amesema kwa mwaka watoto elfu 50 wanakufa kati ya vizazi hai 2,200,000 ambapo asilimia 80 ni wenye uzito pungufu.
Amesema kufuataia agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutaka kuanzishwa chumba maalum kwa ajili ya kuhudumia watoto wanaozaliwa na uzito pungufu kutasaidia kupunguza vifo 30,000 kwa mwaka.
Nae,Daktari wa watoto kutoka chuo Cha MUHAS Dkt. Nahya Salim amesema Tanzania ina mpango mkakati wa kushusha vifo vya watoto wachanga angalau mpaka 17 Kwa vizazi hai 100.000 hadi kufikia 2025.
“Kutokana na ripoti iliyotolewa na Wizara ya Afya ya kushusha vifo vya watoto bado kasi ipo nyuma sana kwa kipindi cha miaka mitano” amesema Dkt Nahya.