OR-TAMISEMI
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe kuhakikisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Ulembwe unakamilika ifikapo Desemba 30, mwaka huu ili unapoanza mwaka mpya wa 2024 wananchi waanze kupata huduma za afya.
Dkt. Dugange ametoa agizo hilo kwenye ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kilipokea kiasi cha sh.Milioni 462 kwa ajili ya ujenzi huo.
“Nimepita kukagua ujenzi wa kituo hiki cha afya nimeridhishwa na ubora wa majengo lakini kituo bado hakijakamilika na kilipaswa kukamilika Septemba mwaka huu lakini kwa sababu ya taratibu za kimanunuzi na mfumo kimechelewa, hivyo nimuagize Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha anasimamia ujenzi huu ukamilike Desemba 30 na Januari mosi, 2024 wananchi waanze kupata huduma.”
“Jambo la pili nataka nijiridhishe kwa sababu fedha iliyoletwa Sh. Milioni 462 ilikua kukamilisha majengo yote na kwa sababu ujenzi umesimama nataka nipate taarifa ya uhakika ndani ya saa 24 kama fedha iliyobaki inatosha kukamilisha majengo haya. Kwa lugha nyingine nisingependa kusikia kuwa fedha haitoshi kwa sababu Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alileta fedha ili kukamilisha kituo hiki hivyo fedha zinapaswa zisimamiwe kwa weledi,” amesema Dkt. Dugange.
Naibu Waziri Dugange amesema kukamilika kwa kituo hiko cha afya kutasaidia wananchi wa Kata hiyo ya Ulembwe kuepuka gharama za kutembea umbali mrefu wa kilometa 30 kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe.
“Tunamshukuru sana Mhe.Rais kwa kutupatia fedha hizi ambazo sasa kituo hiki kitakuwa na jengo la kisasa la upasuaji, jengo la mama na mtoto, jengo la maabara, jengo la kufulia na kichomea taka pamoja na jengo la mtumishi,” amesema Mhe. Dkt. Dugange.