Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
TIMU ya Mpira wa Pete, ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) maarufu kama TMDA QUEENS imeicharaza timu ya TPHPA kwa jumla ya magoli 21 dhidi ya 15 katika mashindano ya SHIMMUTA yanayoendelea Jijini Dodoma.
Mchezo huo ulichezwa siku ya Jumatano tarehe 15 Novemba 2023 saa 10:00 jioni katika uwanja wa Kilimani Park uliopo Dodoma.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo Kapteni wa TMDA QUEENS Halima Sembe ameeleza kuwa timu yake ilijiandaa vyema kupata matokeo katika mchezo huo, ili kujihakikisha nafasi ya kuweza kufuzu hatua za mtoano.
“Tunamshukuru Mungu kwa kupata matokeo katika mechi ya leo.
Tulijipanga kuutawala mchezo kwa kumshambulia zaidi mpinzani kuanzia dakika ya kwanza ili tuweze kupata ushindi wa magoli mengi zaidi lakini wapinzani wetu nao walijitahidi kuonyesha ukomavu wa kutuzuia tukaishia magoli hayo 21. Mchezo huo umeshapita na sasa tunaangalia michezo iliyo mbele yetu ili nayo tufanye vizuri.
Mashindano ya SHIMMUTA yalianza tarehe 12 Novemba, 2023 na yanatarajiwa kuendelea hadi tarehe 25 Novemba, 2023.