NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amezindua rasmi mfumo kwa wafanyabiashara ndogo ndogo(Wamachinga) ambao uwapa fursa ya kuweza kujisajili kwa njia ya simu zao lengo ikiwa ni kutambulika kwa urahisi pamoja na kufahamu aina ya bidhaa wanazoziuza.
Mkuu huyo amezindua mfumo huo wakati wa mkutano maalumu ambao uliandaliwa kwa lengo la kuweza kujadili mambo mbali mbali ikiwemo suala muhimu la wafanyabiashara hao wahame kutoka mfumo wa zamani na kujisajili kwa njia ya kisasa zaidi ili watambulike.
“Kitu kikubwa wafanyabiashara ndogo ndogo natambua mpo wengi lakini suala la kuhakikisha sisi kama serikali tunawatambua ni vema mkajisajili kwa kutumia simu zenu na lengo lake kubwa ni kutambulika mnafanya nini katika shughuli zenu hii itatusaidia kupata na takwimu halisi,”alisema Saimon.
Kadhalika Mkuu huyo aliongeza kwamba ni lazima kujiwekea mipango madhubuti ambayo itaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara kuendesha shughuli zao katika mazingira mazuri na ambayo yametengwa rasmi kwa shughuli zao.
Pia aliongeza serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana bega kwa bega na wafanyabiashara wote wadogo wadogo na kuwawezesha kiuchumi ili wawze kufikia malengo ambayo yamejiwekea ikiwemo kuweza kutambulika na serikali kupata takwimu za idadi yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la umoja wa machinga Mkoa wa Pwani (SHIUMA) Filemon Malinga alibainisha kwamba lengo lao ni kuwahimiza wafanyabiashara wote kujisajili kwa njia ya kisasa zaidi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa endapo wafanyabiashara hao wakiingizwa katika mfumo mpya na kusajiliwa kwa njia ya simu zao itasaidia kupata idadi ya takwimu halisi ikiwemo na aina ya biashara ambazo wanazifanya katika maeneo yao mbali mbali.
“Tumejitahidi kupata wataalamu wa Tehama kutoka taasisi ya TIVA ambapo imeweza kupata fursa ya kuelimisha jinsi ya umuhimu wa wafanyabiashara hao kujisajili kwa mfumo wa kanzi data ambayo hii tutaondoka na ile hali ya kujisajili katika makaratasi,”aliongeza Mwenyekiyi.
Aidha Mwinyekiti huyo hapo awali waliwasajili wanachama wao kwa kutumia makaratasi lakini kutokana na teknolojia ilivyokuwa watajisajili kwa kutumia simu zao za kiganjani ili kuondokana na usumbufu wa hapo awali katika suala zima la ukusanyaji wa taarifa.
Kwa upende wake Mwenyekiti wa soko la Mnalani(Loliondo) Mohamed Mnembwe amesema kwamba utaratibu huo wa wafanyabiashara kuweza kuingia katika mfumo wa kujisajili utasasaidia kujua idadi halisi pamoja na bidhaa wanazouza.
“Leo tumekutana katika huu mkutano ambao umewajumuisha wafanyabiashara ndogo ndogo wa Mkoa wa Pwani na haya maelekezo tuliyopewa na mtaakanu wa Tehama yataweza kutusaidia sisi kama wafanyabiashara “alisema Mnembwe.
Mnembwe alisema kwamba ana imani endapo wafanyabiashara wote wakielimishwa umuhimu wa kujisajili kwq simu kutaweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kutoka na kufanya kazi kwa mfumo wa kidigitali na itasaidia kutambulika.