******************************
Dar es Salaam, Novemba 12, 2019: Jumla ya wachezaji 120 wa gofu kutoka sehemu mbali mbali hapa nchini, wanatarajiwa kuchuana vikali mwishoni mwa wiki katika mashindano ya Waitara Gofu ya mwaka 2019 yanayodhaminiwa na kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).
Mashindano hayo ya siku moja, yatafanyika siku ya Jumamosi katika viwanja vya Gofu vya Lugalo jijini Dar es Salaam.
Akitangaza udhamini huo jijini Dar es Salaam, Meneja masoko wa SBL Anitha Msangi aliwaambia waandishi wa habari kuwa udhamini wa SBL kwenye mashindano hayo maarufu, unalenga kuendeza mchezo wa gofu hapa nchini.
“Kampuni ya SBL kupitia bia yake pendwa ya Serengeti Premium Lager inayofuraha kuwa mdhamini mkuu wa mashindano ya gofu ya Waitara ya mwaka huu. Udhamini huu unaonyesha nia yetu ya dhati ya kuendeleza michezo hapa nchini,” alisema Anitha.
Kupitia bia ya Serengeti Premium Lager, kampuni ya SBL ni mdhamini mkuu wa Timu ya Taifa, Taifa Stars Serengeti na pia inadhamini ligi ya taifa ya wanawake kupitia bia yake ya Serengeti Lite.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa klabu ya Gofu ya Lugalo Brigedia Jenerali mstaafu Michael Luwongo aliishukuru kampuni ya SBL kwa udhamini huo na kuyataka makampuni na taasisi nyoingine kuiga mfano wa SBL na kujitokeza kusaidia michezo wa gofu nchini.
“Tunaishukuru sana kampuni ya SBL kwa mchango wake kwenye kusaidia maendeleo ya michezo hapa nchini na hususani gofu. SBL imekuwa mdhamini mkubwa wa mashindano haya,” alisema.
Mashindano ya Waitara Golf hufanyikja kila mwaka yakilenga kutambua mchango wa Genelrali mstaafu George Waitara aliyekuwa mkuu wa majeshi kwa kuanzisha klabu ya golf ya Lugalo.
Klabu ya Golf ya Lugalo ilianza mwaka 2006 kutokana na mchango mkubwa wa Waitara ambo pia uliendelezwa na Generali Davis Mwamunyange ambaye alimfuatia baada ya kustaafu.