Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika mradi wa Uboreshaji wa Mto Msimbaza unaotegemewa kuanza hivi karibu utatatua changamoto za miaka 100 ijayo na sio baada ya miaka 10 tena tunaanza kukutana na changamoto kama hizi.
Hayo yamesemwa leo tarehe 13.11.2023 wakati wa ziara ya pamoja ya Mawaziri wa Wizara tatu ambazo zimetembelea eneo la Jangwani ambalo limathirika na mvua zinazoendelea kunyesha baada ya Mto Msimbazi kujaa.
Wizara hizo ni Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi pamoja na Wizara ya Fedha.
Amesema tayari Serikali kupitia OR-TAMISEMI imesaini mkataba wa kupata fedha kutoka Benki ya Dunia zitakazo wezesha kutekeleza mradi mkubwa wa uboreshaji wa Bonde la Mto Msimbazi ikiwa ni pamoja na kujenga daraja la juu litakaloanzia eneo la Magomeni hadi njia panda ya Muhimbili (Fire) ambao umepangwa kuanza Februari 2024.
“Katika utekelezaji wa mradi huu lazima tukae wizara zote zinazohusika na wataalamu watupitishe ili tukubaliane namna mradi bora utakaoweza kutatua changamoto za miaka 100 ijayo na sio baada ya miaka 10 tena tunakutana na vitu kama hivi hii sio Sawa.”
“Lazima tukiri kwamba waliotushauri tuijenge Jangwani kwa namna ilivyo sasa walitukosea, lakini tukiri makosa huku tukijisahihisha. Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu tayari imesaini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo ambapo ujenzi unatarajiwa kuanza mapema iwezekanavyo,” alisema Waziri Mchengerwa.
Katika mradi huo TANROAD itahusika moja kwa moja na ujenzi wa daraja hilo na Ofisi ya Rais–TAMISEMI ikihusika uboreshaji wa bonde ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kingo za mto, maeneo ya kupumzikia, kupanda miti na kudhibiti maeneo yote yanayozalisha taka ili siziingie kwenye mto.
Wakati huo huo Waziri Mchengerwa amewataka mameneja wa TARURA wa mikoa kuzitumia vyema mvua zinazoendelea kunyesha nchi nzima katika kufanya ukaguzi wa barabara wanazozisimamia ili kubaini sehemu zinazohitaji ukarabati na kuzifanyia kazi kabla hazijaleta madhara.
Ziara hiyo iliyolenga kutathimini athari zilizotokana na mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam na mikakati ya muda mrefu ya Serikali ya utatuzi wa changamoto hiyo katika maeneo yanayozunguka Mto Msimbazi.
Katika ziara hiyo Waziri Mchengerwa ameambatana na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila pamoja na wataalam mbalimbali kutoka TARURA na TANROAD.