Wauuguzi watarajali kumi na nne (14) wamefanikiwa kuhitimu mafunzo yao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke na kuagwa rasmi leo hospitalini hapo. Watarajali hao wameagwa leo na kupatiwa vyeti vya kuonyesha uhitimu wao.
Katika hafla hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dkt. Joseph Kimaro, amewapa hongera za dhati wahitimu kwa mafanikio waliyopata katika mafunzo yao. Amewasihi kuendeleza juhudi zao katika utoaji wa huduma bora za afya na kuwa watoa huduma wenye upendo kwa kila mgonjwa watakayemhudumia.
Dkt. Kimaro, pia amewataka wataalamu hao wa afya kufuata taratibu na viapo vya uuguzi wanapotekeleza majukumu yao. amesisitiza umuhimu wa kuwa wauuguzi wenye uadilifu, watiifu, na kujituma katika kutoa huduma kwa jamii. Aidha amewataka watarajali hao kuweza kutumia muda wao kujifunza mambo mapya nakuendelea kupata elimu zaidi ili kuweza kutoa huduma bora ya afya.
Nae, Muuguzi Mfawidhi, Nuswe Ambokile amewataka wahitimu hao kuheshimu miongozo ya maadili ya uuguzi na kuwa wachapakazi na waadilifu, Amewataka kufanya kazi kwa usawa na haki, bila kujali hali ya mgonjwa, na kutoa huduma kwa upendo na utu.
Kwa upande wa mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya utarajali ya uuguzi, Bi. Halima Mohammed, amesema hakika amejifunza mambo mengi mazuri na ameahidi kwenda kuyatenda mambo aliyojifunza huko anapokwenda kufanya kazi. Pia amesema kuwa mwanzo aliogopa kuja lakini baada ya kufika na kufanyakazi Temeke ameona yanayo ongelewa kuhusu Temeke sio kweli kwani ina wataalamu walio na moyo wa kujitoa kwaajili ya wagonjwa wao.