Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Joseph Hezron (54) mkazi wa Bukara Wilaya ya Sengerema kwa kosa la kuchoma moto nyumba ya Lucy James (51) ambae ni mpenzi wake mkazi wa Ibisabageni ambapo mali mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya milioni 16 ziliteketea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 10, 2023 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa, amesema tukio hilo lilitokea Novemba 9, 2023 baada ya Joseph Hezron kumtuhumu Lucy James kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Jelemia Kamambi (53).
Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa mwanaume ambaye alikuwa anamtuhumu hakuwa mpenzi wa Lucy Hezron bali alikuwa ni Kaka yake.
“Baada ya kuchoma moto nyumba ya mpenzi wake aliyekuwa anaeishi naye katika nyumba hiyo Joseph Hezron alijaribu kujiua kwa kujijeruhi na kitu chenye ncha Kali shingoni”, amesema Mutafungwa
Amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na uokoaji pamoja na wananchi walifanikiwa kuzima moto huo kabla haujaleta madhara makubwa,pia walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa aliyekuwa amejificha porini baada ya kutenda uhalifu huo ambapo kwa sasa anatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Sengerema.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kutafuta njia sahihi ya kutatua migogoro hususani ya kimahusiano, pia wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.