NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka amezindua shule ya msingi na awali ya Mkombozi iliyopo kata ya Pangani na kuchangia madawati 20 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu.
Katika halfa za uzinduzi wa shule hiyo zimeudhuliwa na viongozi mbali mbali wa serikali,madiwani pamoja na viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) ambao walifika kushuhudia jinsi ya utekelezaji wa ilani unavyofanyika.
Mbunge Koka alisema kwamba lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha inaweka mazingira bora katika kuboresha sekta ya elimu kuanzia ngazi za awali hadi za juu.
“Nimekuja hapa kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa shule hii ya msingi na awali ya mkombozi hakika nimefarijika sana kwa hatua hii kwani watoto wetu watapata elimu kuanzia ngazi ya awali na msingi,”alisema Koka.
Aidha Koka alisema kwamba kwamba pamoja na kuzindua shule hiyo atahakikisha anaweka miundombinu mizuri katika shule hiyo kwa ambayo itawasaidia wanafunzi waweze kusoma kwa bidii na kuongeza ufaulu
Sambamba na hilo Mbunge huyo alibainisha kuwa anaweka mipango mizuri kwa kushirikiana na mamlaka husika katika kuweka huduma za msingi ikiwemo maji na umeme.
Pia alisema kwamba amechaguliwa kuwaongoza wananchi wa Jimbo la Kibaha mjini hivyo ataendelea kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Pia amechangia madawati 20 kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi hao wasome katika mazingira rafiki na kuondokana kusoma katika hali ya msongamano.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Mkombozi Medard Rweyemamu alimpongeza Mbunge huyo kwa kuboresha zaidi sekta ya elimu.
Alisema kwamba msada wa madawati hayo waliyopatiwa yatakwenda kuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi hao kuondokana na changamoto ya kusoma kwa mlundikano.
Naye Diwani wa Kata ya Pangani Agustino Mdachi aliongeza kuwa kuzinduliwa kwa shule hiyo ni moja ya hatua kubwa katika kuwasaidia wanafunzi katika kupata elimu.
Aliongeza kuwa ana imani kukamilika kwa shule hiyo ya msingi na awali mkombozi kutaweza kuwaletea maendeleo katika kuwapatia watoto hao elimu.
Nao baadhi ya wananchi wa kata ya Pangani wameipongeza serikali ya awamu ya sita pamoja Mbunge Koka kwa juhudi za kuweka mazingira mazuri ya kuboresha sekta ya elimu na kufanikisha ujenzi wa shule hiyo ya mkombozi.