Na Sophia Kingimali
MAKAMU wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Phumzile Mlambo Ngeuka amewataka wanaharakati wa kifeminia nchini kujikita katika kuelimisha kuhusu ulinzi wa mtoto wa kiume kwa mustakabali wa haki na usawa wa jinsia huku akitoa rai kwa wazazi kuanza kukomesha mfumo dume kuanzia ngazi ya familia.
Amesema ipo haja ya kuwa na majukwaa ya wanaume nchini yenye kueleza yanayowahusu lakini pia kujikita na kuchukua hatua za kupinga ukatili wa kijinsia, wanaopinga ubaguzi dhidi ya wanawake na wanaokataa ndoa za utotoni.
Phumzile amesema hayo novemba 7,2023 jijini Dar es Salaam katika tamasha la 15 la jinsia pamoja na kuadhimisha miaka 30 ya kifeminia la Mtandao wa jinsia nchini (TGNP).
Amesema katika harakati za kukataa ukandamizaji wa aina yoyote pia suala la ulinzi wa mtoto wa kiume halina budi kuzingatiwa kwa kuendeleza ajenda za kumkomboa.
“Wanaharakati wa haki za binadamu msiruhusu aina yoyote ya ukatili kuanzia kuukataa mfumo dume kuanzia katika ngazi ya familia,” amesema Phumzile na kuongeza kuwa ipo haja ya kuwepo mabadiliko ya kisera na sheria lakini pia jamii kubadilika.
Aidha alisema mfumo dume sio rafiki kwa wanawake na hata wanaume na umekuwa ukiendeleza ubaguzi hivyo ni muhimu kwa wanaume na watoto wa kiume kuwa miongoni mwa harakati za kuupinga kwani karne hii inahitaji wanaume wenye mshikamano na wenza wao.
Kadhalika alisema tamasha la jinsia litumike pia kuwashirikisha wanaume
.Awali akizungumza, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gema Akilimali amesema licha ya Mtandao huo kuadhimisha miaka 15 za usawa wa kijinsia lakini changamoto bado ni nyingi na mshikamano na serikali unahitajika zaidi kwa sasa kuliko huko walikotoka.
Amesema katika tamasha hilo la siku nne watatoka na maazimio ya jumla kwani upo mchango wa TGNP katika harakati mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TNGP, Lilian Liundi amesema Tamasha la jinsia ni jukwaa la kuleta sauti kwa pamoja lenye lengo kujadili kwa pamoja na kupanga mikakati endelevu.
“Tamasha hili ni la 15 tangu kuanzishwa limeweza kuwa na washiriki 2000 hadi 5000 kwa tamasha moja limewafikia watu zaidi ya 35000,”amesema Liundi.
Amesema tamasha hilo limewaleta watu kwa pamoja ukanda wa Afrika na wameendelea kusimama kwenye misingi ya waasisi wao.
Aidha amesema TGNP imejengwa katika misingi imara ya haki na kuondoa mifumo kandamizi.