VICTOR MASANGU,KIBAHA
Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa kiasi shilingi milioni 252 kwa ajili ya ukarabati wa daraja la mto Mpiji ili liweze kuwasaidia wananchi wa kata ya pangani kuvuka kwa urahisi hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Koka ametoa pongezi hizo wakati alipowatembelea wananchi wa kata ya pangani kwa lengo la kuweza kujionea hali halisi ya miundombinu wa daraja hilo pamoja na kuzungumza na wananchi ili kuwaeleza fedha ambazo zimetolewa na serikali ya awamu ya sita.
Koka ambaye pia aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikson Saimoni pamoja na wataalamu mbali mbali kutoka Tarura lengo ikiwa ni kuona namna ya kufanya ili kulitengeneza daraja hilo la muda liweze kupitika kwa urahisi katika kipindi chote.
“Kiukweli nipende kumpongeza kwa dhati Rais wetu wa awamu ya sita kwa kuweza kutukubalia kutupatia fedha hizi kiasi cha shilingi milioni 252 ambazo tayari zimeshakuja kwa ajili ya kukarabati baadhi ya maendeo ambayo yameharibika ikiwemo kingo,mbao na sehemu nyingine,”alisema Koka.
Kadhalika Mbunge huyo alibainisha kwamba katika enjoy hilo daraja ambalo limejengwa kwa sasa ni la muda tu lakini kitu ambacho wanachokifanya ni kufanya matengenezo kupitia fedha walizozipata ili wananchi waweze kupata fursa ya kupita kwa urahisi.
Aidha Mbunge huyo alisema lengo lake kubwa ni kushirikiana na mamlaka husika ikiwemo Tarura kwa ajili ya kuhakikisha hatua za haraka zinafanyika mapema ili kudhibiti uharibifu ambao unaendelea katika maeneo ya pembeni ya daraja hilo.
“Kimsingi kitu kikubwa ambacho tunakifanya kwa sasa ni kufanya upembuzi wa kina ili kulidhibiti daraja hili lisiweze kubomoka kwani ni kiunganishi muhimu sana kwa wakazi wa kata ya pangani na maeneo mengine ya jirani kwa wen zetu wa Dar es Salaam,”alisema.
Kwa upande wake Meneja wa Tarura Wilaya ya Kibaha Samwelu Ndoveni amekiri kupokea kiasi cha shilingi milioni 252 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya haraka zaidi katika daraja hilo la mpiji ili lisiweze kuharibika zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikson Saimon alisema kwamba wananchi wa kata ya Pangani ambao wanatumia daraja hilo wamekuwa wakipata adha kubwa hasa katika kipindi cha mvua na kwamba fedha hizo zitakwenda kutumika kwa manufaa.