Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema kuwa Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi tilioni 47.424 katika mwaka 2024/2025.
Dkt. Nchemba alisema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25.
Alisema kuwa makusanyo hayo yatatokana na vyanzo mbalimbali yakiwemo mapato ya ndani, michango kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na mikopo.
“Mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa shilingi tilioni 34.436 sawa na asilimia 72.6 ya bajeti yote, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi tilioni 4.291 sawa na asilimia 9.0 ya bajeti. Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 6.141 kutoka soko la ndani na shilingi trilioni 2.555 kutoka soko la nje”, alieleza Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Maoteo ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 yamezingatia mwenendo wa ukusanyaji mapato, matarajio ya ukuaji wa uchumi, hali ya uchumi wa dunia pamoja na mikakati ambayo Serikali inaendelea kuchukua katika kuongeza mapato ya ndani.
Kuhusu matumizi ya Serikali kwa mwaka 2024/2025, Dkt. Nchemba alisema Serikali inakadiria kutumia shilingi tilioni 47.424 kati ya kiasi hicho, deni la Serikali shilingi tilioni 12.101, mishahara shilingi tilioni 11.774 na uendeshaji wa shughuli za Serikali shilingi tilioni 8.223.
‘’Matumizi kwa ajili ya programu na miradi ya maendeleo ni shilingi tilioni 15.325 ikijumuisha ruzuku ya maendeleo ya Elimu msingi na Sekondari bila ada na Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu”, aliongeza Dkt. Nchemba.
Alifafanua kuwa Makadirio hayo yamezingatia mahitaji ya kugharamia deni la Serikali, mishahara ya watumishi wa umma, uendeshaji wa miradi iliyokamilika ikiwemo miundombinu ya elimu, afya, umeme na maji, ugharamiaji wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Alisema kuwa misingi iliyotumika katika kuandaa shabaha za uchumi jumla ni pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara, kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili kama ukame, vita, magonjwa ya mlipuko na mafuriko.
Dkt. Nchemba alieleza misingi mingine iliyotumika kuandaa shabaha za uchumi jumla ni kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya fedha na bidhaa, kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuendelea kuimarika kwa utoshelevu wa chakula nchini na uwepo wa amani, usalama, utawala bora, umoja, utulivu wa ndani na nchi jirani.
Alisema kuwa kutokana na uchambuzi huo, Pato Halisi la Taifa linakadiriwa kukua kwa asilimia 5.2 mwaka 2023 na kuongezeka hadi asilimia 5.8 mwaka 2024.
Aidha alisema kuwa Mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia 3.0 hadi 7.0 katika kipindi cha muda wa kati na Mapato ya kodi kufikia asilimia 12.4 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2024/25 kutoka uwiano halisi wa asilimia 11.9 uliofikiwa mwaka 2022/23.
Mhe. Dkt. Nchemba alieleza kuwa nakisi ya bajeti ikijumuisha misaada kuwa asilimia 2.2 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 kutoka matarajio ya asilimia 2.7 ya mwaka 2023/24, kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4) na Kuimarika kwa viashiria vya ustawi wa jamii.
Bunge linatarajia kujadili Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 kwa siku tano kuanzia leo.