Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Nov 5, 2023
BAADHI ya viongozi walioshirikiana na madalali ,wamejipatia zaidi ya kiasi cha sh.milioni 900, ikiwa ni sehemu ya kuuzia watu kitapeli viwanja eneo la Serikali la Mitamba ,shamba namba 34 ,Kata ya Pangani, Halmashauri ya Mji Kibaha ,mkoani Pwani.
Fedha hizo zimetafunwa kinyume cha sheria na kuwasababishia wananchi waliowatapeli wakihangaika huku wasijue namna ya kupata haki yao.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alitoa taarifa hiyo kwenye kikao kilichowahusisha waandishi wa habari wa mkoa huo, wakuu wa wilaya, watalaam na wakurugenzi kutoka Halmashauri mbalimbali, kilichokuwa na lengo la kuwasilisha utatuzi wa migogoro.
Alisema ,shamba la Mitamba Kibaha lipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kusimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) .
“Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipewa shamba la hekta 4,000 na Wizara ilikubali kuipatia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kiasi cha hekta 2,963 bila malipo yeyote na Wizara ikabaki na hetka 1,037 ila pamoja na kugawa eneo hilo bado wamevamia kipande kidogo kilichobaki”alieleza Kunenge.
“Tatizo lililopo ni wananchi kukiuka sheria, hawafuati sheria ,wengi wamekuwa wakivamia maeneo ambayo yanamilikiwa kihalali na Serikali, mtu mmoja ama wawekezaji wakati yanamilikiwa kihalali” alisisitiza Kunenge.
Hata hivyo, aliwataka wananchi waliowatapeli wakawashtaki Mahakamani waliowatapeli ili sheria ichukue mkondo wake na kupata haki zao.
Kunenge alieleza kuwa, Serikali haijui waliowatapeli kwa mtu mmoja mmoja hivyo hatua inayochukua ni kuwasaidia kuwaunganisha na wanasheria kwa wale ambao watashtaki na kukosa msaada wa kisheria.
Vilevile Kunenge ,alishatoa muda wa siku 14 kukamatwa viongozi hao wapatao 24 wakiwemo mabalozi, wenyeviti wa mitaa, watendaji walioshirikiana na madalali waliohusika kuwauzia wananchi viwanja katika eneo la shamba hilo na uchunguzi unaendelea.
“Bado uchunguzi unaendelea na wahusika wanahojiwa ,bado tunapisha uchunguzi kisha nitaleta matokeo ya uchunguzi huo na kueleza hatua walizochukuliwa waliobainika na utapeli huo”alieleza Kunenga.
Kunenge alieleza, orodha ya majina ya viongozi na madalali hao ameyakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Mkuu huyo wa mkoa pia alitoa maelekezo kwa Halmashauri ya Mji Kibaha na wataalamu kupima eneo la shamba 34 la Mitamba ili kubaini mipaka yote na matumizi yake ndani ya siku 60 .
Katika hatua nyingine, Kunenge alieleza ipo migogoro kati ya kambi za Jeshi na wananchi ,na amewashauri wananchi wasiingie maeneo hayo kwani yana taratibu zake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nikkison Saimon aliwaasa wananchi wafuate sheria,msingi mkubwa unaonesha watu wanafanya jinai hali inayochochea migogoro ya ardhi.
Nae Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha, Aron Shushu alieleza, kiwanja hicho kilipimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji , ambapo mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo.