Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania CTI Bw. Leodgar Tenga akizungumza wakati wa mafunzo hayo kwa wafanyabiashara Wenye Viwanda nchini.
……………………..
TUME ya Ushindani Nchini (FCC), imewataka wafanyabishara na wamiliki wa viwanda nchini kutoa taarifa za kuwafichua watu wasio waaminifu ambao wanaingiza na kutengeneza bidhaa bandia nchini kwani zinahujumu uchumi na kuondoa ushindani.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam leo Novemba 03, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara.
Amesema uwepo wa bidhaa bandia nchini kuna athari kubwa ikiwemo kuondoa ushindani sokoni na kupoteza mapato.
“Serikali ya Rais Dk.Samia inategemea kodi zinazolipwa na sisi wafanyabiashara katika kuleta maendeleo, hivyo ni vyema tukahakikisha tuna toa taarifa za watu hao kuwadhibiti,” amehimiza.
Erio aliwataka wafanyabishara na wamiliki hao wa viwanda kuchangamkia fursa ya soko huru la Afrika ambapo Tanzania ni miongoni mwa wanachama katika soko hilo la Africa lililofunguliwa hivi karibuni wafanyabiashara watapata faida zaidi kwa kuuza na kutangaza biashara zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa udhibiti wa bidhaa Bandia wa FCC, Khadija Ngasongwa amesema kuna athari kubwa za matumizi ya bidhaa hizo kwani faini zake ni kubwa kwa wale wanaobainika kuhusika lakini zinapoteza pato la taifa na kudidimiza uchumi.