Mhe. Balozi Mbarouk alitoa kauli hiyo Bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi aliyetaka kujua Tanzania inanufaika kiasi gani katika uuzaji wa bidhaa na huduma katika maeneo ambayo Jeshi la Tanzania linafanya ulinzi wa amani.
Balozi Mbarouk amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kwenye jitihada mbalimbali za kutafuta amani duniani kama ilivyoainishwa katika Sera ya Mambo ya Nje 2001 na yapo manufaa makubwa katika ushiriki huo.
“Ushiriki wa Tanzania katika Misheni za Ulinzi wa Amani umekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo; Walinda amani wetu kufaidika na mafunzo ya ziada ambayo yanawajenga na kuwaimarisha,” alisema Balozi Mbarouk
Ametaja faida nyingine nchi inayopata kuwa ni pamoja na ajira za kiraia kwa watanzania na kudumisha utamaduni hususan kukua kwa lugha ya Kiswahili na kutolea mfano katika eneo la DRC, Lebanon na Darfur kumekuwa na ongezeko la matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Mhe. Balozi Mbarouk amesema mbali na manufaa yaliyoainishwa, zipo fursa za kiuchumi ambazo nchi inazipata katika shughuli za ulinzi wa amani.
Balozi Mbarouk ametaja fursa hizo kuwa ni biashara ya bidhaa zinazotumiwa na vikosi vilivyopo katika Misheni kama chakula, mavazi, vinywaji, vifaatiba na dawa.
“Fursa nyingine ni usafirishaji wa mizigo, ujenzi wa majengo yanayohamishika, vifaa na huduma za TEHAMA na kuongeza kuwa Tanzania inaweza pia kuuza teknolojia ya kutumia panya katika kubaini na kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini kama fursa za kiuchumi”, alisema Mhe. Balozi Mbarouk.