Na Elinipa Lupembe – ARUSHA
Mkoa wa Arusha kwa sasa unahitaji mpango mkakati wa uwekezaji mkubwa kiseta, hususani katika miundombinu ya barabara, makazi na rasilimali watu ili kuboresha sekta ya utalii na kumudu kuwahudumia wageni pamoja na kukidhi matakwa ya wageni wote.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, akiwataka wadau na wakazi wa Arusha, kuungana kuwa na mpango endelevu wa kuwekeza kwenye katika sekta zote zinazoweza kulisha sekta ya utalii.
Ameweka wazi kuwa, serikali imetoa fedha za mradi mikubwa ya kimkakati wa Jiji la Arusha ili kuboresha miundombinu na kuwataka wadau na wakazi wa mkoa huo kutumia fursa kuwekeza kwenye sekta zote zinazolisha sekta ya Utalii.
Amefafanua kuwa, Utalii ndio muhimili wa uchumi wa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla, hivyo kunahitajika, uwepo wa miundombinu ya uhakika, kwa kujenga hoteli za kutosha zenye hadhi, barabara za kupitika kipindi chote pamoja na kuwa na rasilimali watu ya kuwahudumia wageni hao.
Ameongeza sasa mkoa umefunguka kiuchumi, unapokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo kuna uhitaji wa kufanya uwekezaji mkubwa, utakaowezesha kumudu upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wageni wote kwa wakati kwa viwango vinavyokidhi matakwa ya wageni.
“Kwa sasa ‘season’ za utalii zinungana kila wakati tunapokea wageni wa ndani na nje ya nchi wakifika hapa kwa hughuli mbalimbali, wapo wanaokuja kwa mikutano na kutembelea vivutio vya utalii, lakini wapo wanaokuja kwa kutalii moja kwa moja na wote wanahitaji kupata huduma stahiki zinazokidhi mahitaji yao, tunahitaji kujipanga vema ili kumudu kuwahudumia bila kuelemewa na waondoke wakiwa wameridhishwa na huduma hizi” Amesema Mongela
Aidha amewataka wakazi wa mkoa wa Arusha kuwa tayari kupokea wageni wengi na kuendelea kuwasihi watu wote kuchangamkia fursa hiyo kujipatia vipato ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, wa mkoa kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mhe. Mongella amethibitisha kuwa Filamu ya Royal Tour iliyofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya Utalii,sekta ambayo ndio muhimili mama wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
“Kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Arusha, tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kufufua Utalii nchini sekta ambayo ilikumbwa na changamoto kubwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19.