Na Eleuteri Mangi, WUSM
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amemwagiza Mkadarasi Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) anayejenga Kituo cha michezo na eneo la kupumzikia wananchi jijini Dodoma, kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Naibu Waziri Mwinjuma ametoa agizo hilo wakati wa ziara katika Mradi huo, Oktoba 31, 2023 katika eneo la Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
“Nimetembelea kukagua mradi huu wa ujenzi wa kituo cha michezo hapa Dodoma, huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametuelekeza Wizara kujenga vituo vya michezo na maeneo ya kupumzika wananchi hapa Dodoma na Dar es Salaam” amesema Naibu Waziri Mwinjuma.
Mhe. Mwinjuma amesema mkandarasi huyo anawajibika kusimamia na kufuata mpango wa manunuzi waliojiwekea pamoja na kuongeza idadi ya wafanyakazi, ili kufikia malengo ya Serikali na kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kwa awamu ya kwanza ifikapo mwezi Machi 2024.
Kwa upande wake Meneja Mradi huo kutoka BCEG Li Liang amesema watasimamia na kufanya kazi kulingana na mkataba huo pamoja na maelekezo ambayo viongozi wanayatoa ili kukamisha kazi hiyo kwa wakati.