Na Sophia Kingimali.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoa wa Pwani imetoa wito kwa wananchi na taasisi za serikali na sekta binafsi kuendelea kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya rushwa na madawa ya kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Pwani Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Pwani Sadiki Alli amesema wamekua na mikakati mingi ambayo wameiweka ili kuhakikisha wanalimaliza suala la rushwa katika mkoa huo.
Amesema wananchi wanapaswa kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili thamani ya fedha ionekane na miradi hiyo itekelezwe kwa kiwango kilichokusudiwa.
“Pia niwaombe wananchi kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa endapo mtavishuhudia au kusikia ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria”amesema Alli.
Aidha Alli ametoa onyo kwa watakaoharibu miradi ya maendeleo kuwa hawatawafumbia macho bali hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya takukuru kupitia mpango wake wa TAKUKURU RAFIKI kubaini rushwa nyingi zinazotokea kwenye mitaa na kusababisha watu wengi kukosa haki zao za msingi.
Akizungumzia swala hilo Alli amesema kupitia programu hiyo wameweza kuokoa shilingi milioni nne za serikali ya kijiji cha Kanga kilichopo Mafia ambazo zilichukuliwa na afisa mtendaji wa kata hiyo ya Kanga.
Amesema fedha hizo ambazo ni mali ya serikali ya kijiji zilitokana na mauzo ya kiwanja cha ufukweni(Beach Plot)ambapo fedha hizo zilikua ni tozo ya asilimia 5 ya mauzo ya kiwanja hicho.
Amesema afisa huyo baada ya kupokea fedha hizo hakuziwasilisha ofisini wala kuweka kwenye akaunti ya benki ya kijiji badala yake alitumia kwa manufaa yake binafsi.
“Kwenye mkutano wa TAKUKURU RAFIKI wananchi waliibua kero hiyo makubaliano yaliwekwa kuwa tufuatilie na ikibainika ni kweli basi afisa huyo azirejeshe uchunguzi ulifanyika na ikabainika ni kweli na tayari fedha hizo zimesharudishwa kwenye akaunti ya kijiji”amesema Alli.
Akizungumzia uzuiaji wa rushwa amesema wamefanya ufuatiliaji wa miradi 48 ya maendeleo yenye thamani ya bilion 9,598,292,084.95 katika sekta za kimkakati ambazo ni Elimu,Afya,Maji na Barabara.
Amesema kufuatia ufuatiliaji wa miradi hiyo,baadhi ya miradi ilikua na mapungufu hivyo hatua mbalimbali zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kurejesha fedha zilizotumiwa vibaya kutoka kwa wakandarasi ambao walikua wanatekeleza miradi hiyo.
Sambamba na hayo Alli Amesema wameweka mikakati kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba ili kuendelea kuboresha huduma zao na kuhakikisha swala la rushwa linakwisha.
Ameongeza kuwa moja ya mkatati wao ni kuendelea kutekeleza programu ya TAKUKURU RAFIKI na kampeni ya kutokomeza rushwa na matumizi ya madawa ya kulevya ambapo kampeni hiyo ilizinduliwa kwa kushirikiana na tume ya kudhibiti madawa ya kulevya ambayo itatekelezwa kuanzia shule za msingi,sekondari na vyuo.
Amesema pia wataendelea kufanya ufuatiliaji na chambuzi za mifumo kwa lengo la kuziba mianya ya rushwa itakayobainika lakini pia kuendelea kukagua utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo katika mkoa huo.
Ameongeza kuwa pia wataendelea kuelimisha umma wa watanzania juu ya madhara ya rushwa ili wafahamu nafasi zao katika mapambano dhidi rushwa kwa makundi yote katika jamii.
“Lakini pia mkakati wetu mwingine ni kuendelea na uchunguzi wa vitendo vya rushwa na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale watakaobainika kutenda makosa ya rushwa”ameongeza Alli.