Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mgeni rasmi) akikata utepe wakati wa uzinduzi wa Mradi wa kufua Umeme Ijangala Kijiji cha Masisiwe, Wilayani Makete, mkoani Njombe tarehe 27/10/2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiteta jambo na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Umeme Ijangala, Kijiji cha Masisiwe, Wilayani Makete, mkoani Njombe tarehe 27/10/2023.
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Tandala Dayosisi ya Kusini kati, Wilayani Makete, Mkoani Njombe baada ya uzinduzi wa Mradi wa kufua Umeme Ijangala tarehe 27/10/2023
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga akisalimiana na Mke wa Makamu wa Rais Mama Jenisia Mpango, wakati wa Hafla ya uzinduzi.wa Mradi wa kufua Umeme Ijangala Mkoani Njombe 27/10/2023.
……………………………..
*Mradi kuwa chachu ya shughuli za kiuchumi Njombe.
*Awataka wadau kujitokeza kuwekeza kwenye miradi ya Nishati
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango tarehe 27, Oktoba 2023 amezindua rasmi Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Ijangala wa kW 360 ,unaomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kusini Kati katika kijiji cha Masisiwe Wilaya ya Makete Mkoani Njombe.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Dkt. Mpango ameelezea kufurahishwa kwake na uwepo wa Mradi, na kuwataka Wadau wengine kujitokeza kuwekeza kwenye miradi ya namna hiyo katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wa bei nafuu.
“Mradi huu umegharimu takribani shilingi bilioni 3 milioni 841. Kiasi cha pesa hizo, milioni 997 zimefadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), pamoja na Benki ya Maendeleo (TIB) kutoa Dola za Kimarekani 850 kwa mkopo wenye riba nafuu.” Alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amesema, umeme ni kichocheo cha maendeleo ya watu kwa kuwa bidhaa za mazao ya misitu, kilimo, ufugaji na uvuvi lazima zisindikwe kwa kutumia nishati ya uhakika na ya bei nafuu.
“Sasa ili tufike hapo, tunahitaji uwekezaji imara na katika uzalishaji, usafirishaji na nishati ya umeme katika maeneo ya uzalishaji na usindikaji wa bidhaa”. Amesema Mhe. Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Nishati kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa Mradi wa Rumakali ili kuongeza upatikanaji wa Umeme Wilayani Makete.
Akizungumza wakati wa Hafla hiyo. Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa, Wizara ya Nishati inaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na Umeme kwa wakati na kuwa kwa Wilaya ya Makete wanakaribia kumaliza kupeleka umeme kwa vijiji vyote 98
“Tunategemea hadi kufika terehe 30/10/2023 tutakuwa tumepiga hatua Ili Megawati 80 zote za mradi wa Rusumo ziweze kuingia kwenye Gridi ya Taifa”
“Kupitia REA na TANESCO tunatekeleza miradi mbali mbali ya nishati ikiwemo miradi ya kuzalisha pamoja na kusafirisha umeme sio tu ndani ya nchi yetu lakini Kwa kuunganisha nchi nyingine zikiwemo Zambia, Kenya, Uganda, Burundi na Malawi.” Amesema Naibu Waziri Kapinga.
Awali, akizungumza katika hotuba yake kwa mgeni rasmi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu wa Dayosisi ya Kusini Kati, Askofu Wilson Sanga alieleza kuwa, Mradi ulianza rasmi kwa tafiti mbalimbali mwaka 2010, lakini ujenzi ulianza rasmi Machi 2021 kama shughuli ya kwanza ya Nishati Lutheran (DKK) Investment Limited, kampuni iliyoanzishwa na Dayosisi na kusajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Kwa sasa mradi unazalisha umeme wa kilowati 360 na umeunganishwa na Gridi ya Taifa (National Grid) kwa kufuata makubaliano ya kimkataba kati ya TANESCO na Nishati Lutheran (DKK) Investment Limited yaliyosainiwa Desemba 2020, kufuata fursa zilizopo kwenye chanzo ingawa kinaweza kutoa umeme wa hadi megawati 2, iwapo mitambo itaongezwa”. Amekaririwa Askofu Sanga.
Askofu Sanga amesema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa ruzuku na imeendelea kuchangia sehemu ya gharama za ujenzi ambapo jumla ya shilingi za kitanzania milioni 997.5 zimetolewa pamoja na mkopo nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya TIB (Dola za Marekani 400,000) sawa na zaidi ya milioni 850 fedha za kitanzania.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Viongozi wa Kidini na wakazi wa Makete.