Na Elinipa Lupembe – Arusha
Watumishi wa Afya mkoani Arusha wametakiwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa ili wananchi wavutiwe kwenda kutibiwa kwenye vituo vya afya na hospitali zinazojengwa na serikali.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella wakati akiwajulia hali wagonjwa waliolazwa kwenye wodi ya kina mama Kituo cha Afya Endabashi, wilaya ya Karatu.
Amewasisitiza watumishi wa Afya mkoani humo, kujipanga kutoa huduma bora kwa wagonjwa ili wananchi wavutike kutumia vituo vya Serikali, na kuongeza kuwa Serikali imeajiri watalamu wenye sifa hivyo wanalo jukumu la kutoa huduma kwa weledi na ufanisi mkubwa kwa kuweka mbele uzalendo na huruma kwa wagonjwa.
“Madaktari na Wauguzi mnafanya kazi ya kuokoa maisha ya watu, mnayo dhamana ya maisha yetu, Serikali imewapa dhamana kubwa, fanyeni kazi kwa weledi, tumieni muda wenu kutoa huduma rafiki, kuwajali wagonjwa ndio msingi wa huduma bora kwa mgonjwa” Amesema Mhe. Mongella.
Ameongeza kuwa endapo Madaktari na Wauguzi hamtatoa huduma bora kwa wagonjwa, serikali itakuwa inapoteza muda kuwekeza fedha nyingi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuwaagiza kufanya kazi yao vizruri ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali ya upatikanaji na utoaji wa huduma za afya kwa watanzania wote.
Akiwa Kituoni hapo Mhe. Mongella amewataka wananchi kuendelea kutumia vituo vya afya vya serikali kwa kuwa vinatoa huduma kwa gharama nafuu huku Serikali ikiwa inaendelea kuboresha miundombinu ya vituo, vifaa tiba pamoja na watoa huduma ili kuhakikisha utoaji na upatikanji wa huduma bora kwa wananchi hasa waishio maeneo ya vijijini.
Naye Kaim Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Endabash Dkt. Daniel Kilenge amesema kuwa, wanathamini kazi kubwa na nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita ya kuboresha sekta ya afya kwa upana na ukubwa wake, na kuahidi kujituma katika kufanya kazi kwa weledi zaidi kwa kuzingatia umuhimu wankazi ya udaktari kwa wagonjwa.
Aidha Dkt. Kilenge amekiri kufanyia kazi na kurekebisha mapungufu yote ambayo mkuu wa mkoa ameelekeza ili kutoa huduma bora na kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita.
Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa iliyopokea fedha za kujenga hospitali za wilaya ya Karatu, Longido na kufanyika ukarabati mkubwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Monduli huku Vito vya Afya na Zahanati zikijengwa kwa wingi