Na Sophia Kingimali
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA)leo Oktoba 27, 2023 imepokea makontena 9 ya vifaa kwa ajili ya kuboresha mawasiliano kati ya waongoza ndege na rubani ambapo vifaa hivyo vinaenda kufungwa katika vituo 18 nchi nzima.
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kupokea makontena hayo Mkurugenzi Mkuu Hamza Johari amesema serikali imetenga bilioni 31.5 kwa ajili ya kuboresha mawasiliano katika viwanja Vya ndege lengo kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa viwanja lakini pia kuongeza wigo wa usafiri wa Anga
“Nimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga kiasi cha bilion 31.5 kwa ajili ya kuboresha mifumo ya Mawasiliano kwenye viwanja vya ndege kati ya waongoza ndege na rubani”
Amesema baada ya serikali kutoa fedha walitangaza zabuni shindanishi za kimataifa na kupatikana mzabuni kutoka Norway na Italy ambae ameshinda na ndio aliyeleta makontena hayo ya mitambo.
Amesema wakiwa wanajiandaa na maboresho hayo TCAA iliwapeleka wataalam wake 24 nchini Italy na Norway kwa ajili ya kupata mafunzo ya mitambo hiyo.
Akitaja vituo ambayo itafungwa mitambo hiyo ni pamoja na kiwanja cha ndege cha kimataifa Julius Nyerere,Pemba,uwanja wa Abed Amani Karume Zanzibar, Songwe,Mwanza,Tabora,Kigoma, Dodoma Mtwara,Tanga,Kilimanjaro na Arusha.
Amesema baada ya kufungwa kwenye viwanja hivyo pia kutakua na vituo vya kurefusha na kukuza mawasiliano ya sauti ambavyo vituo hivyo vutakua 18 nchi nzima.
Ametaja vituo hivyo ambavyo ni Kiuwe,Matogoro Songea,Mbunga Mtwara,Mwasenyi Rufiji,Michakani Pemba,Arusha,Oldeianamalanja Ngorongoro,kwejunga Tanga,Gairo Morogoro,Dodoma,Mwisi Tabora, Kigoma,Nyamanya Bihalamuro,Mbiso Katavi,kituro,Muganza Butiama,Mara na Mugumu.
“Tunachotarajia baada ya kufunga mitambo hii ni mawasiliano kati ya marubani na waongoza ndege katika anga lote la Tanzania na anga la juu la nchi ya Burundi yatakuwa yameboreka kwa mujibu wa viwango vya kimataifa”amesema Johari
Ameongeza baada ya kufungwa mitambo hiyo huduma za usafiri wa anga zitaimarika maradufu na kuchagiza idadi ya miruko ya ndege katika nchi na idadi ya mashirika ya ndege yanayokuja nchini lakini pia idadi ya abiria na kusapoti royal tour kwa kupata idadi kubwa ya watalii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Huduma za Uongozaji ndege Frola Mwanshinga amesema kufungwa kwa mitambo hiyo kutaboresha huduma na kuongeza idadi ya kampuni za ndege nchini.
“Tunategemea mifumo yetu kuwa sambamba na mifumo ya nchi nyingine jirani na kuweza kufanyakazi kwa pamoja”amesema Mwanshinga
Mitambo iliyopokelewa ni radio za kidigital za masafa ya juu inayojulikana Kama VHF,mitambo ya kurekodi mifumo ya mawasiliano ya sauti(digital voice Recording System) pamoja na mifumo ya kuunganisha ya kuangalia mawasiliano.