Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizindua Chama cha Wazee Wanaume Tanzania katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma Oktoba 27, 2023.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wazee wakati wa uzinduzi wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma Oktoba 27, 2023.Picha zote na Kitengo cha Mawasilano Serikali WMJJWM
……..
Na WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amevitaka Vyama vinavyoshughulika na masuala ya Wazee nchini kufanya kazi kwa karibu na Mabaraza ya kisera ya Wazee kupitia mwongozo wa Kitaifa.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania iliyofanyika jijini Dodoma Oktoba 27, 2023, Waziri Dkt. Gwajima amesema mwongozo huo uliozinduliwa Oktoba 6, 2023 kwenye maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Kitaifa Mkoani Geita unaelekeza namna ya kuratibu masuala yote ya wazee kwa ushirikiano wa Mabaraza ya Wazee na Vyama vya Wazee.
Waziri Dkt. Gwajima amesema mwongozo huo uliozinduliwa Oktoba 6, 2023 kwenye maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Kitaifa Mkoani Geita unaelekeza namna ya kuratibu masuala yote ya wazee kwa ushirikiano wa Mabaraza ya Wazee na Vyama vya Wazee.
Aidha Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza Asasi na Vyama vyote vya Wazee nchini kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sera, Sheria, Miongozo na Mipango ya Serikali huku wakizingatia Katiba zao bila kuingilia majukumu ya mamlaka nyingine au vyama vingine pamoja na kuwa na mikakati ya kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao kikamilifu.
Kuhusu malezi ya vijana, Waziri Gwajima amewakumbusha wanaume kuwajibika kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii unaosababishwa na kukosa malezi stahiki.
Ameziahidi Asasi na vyama vyote vya Wazee kuwa, Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano ambapo amezitaja baadhi ya juhudi zinazofanywa na Serikali ni pamoja na Kuunda mabaraza ya ushauri wa masuala ya wazee ambayo ni kiungo cha kisera kati ya jamii ya wazee wa makundi mbalimbali na Serikali.
Aidha, kushirikiana na majukwaa ya wazee kufanya mapitio ya Sera ya wazee ya mwaka 2003 na kuja na rasimu ya sera mpya ya wazee ya mwaka 2023 ambayo iko kwenye hatua za mwisho.
Akitoa salaam za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerard Mongela amewataka wazee kuwa sehemu ya kusaidia maendeleo ya nchi kwa kuendelea kuwa washauri wazuri na kuwafungulia mlango vijana wanaotumikia taifa.
“Viongozi vijana wanahitaji sana hekima ya wazee, chini ya Uongozi wa Rais Samia mkawe kielelezo, muendelee kutoa ushauri bila kuchoka. Kupitia Chombo chenu, mtumie taaluma zenu muweke kwenye maandishi ili iwe kumbukumbu” amesema Mhe. Mongela
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wazee Wanaume Joseph Laizer amebainisha kwamba Chama hicho kimetokana na kuwa na malalamiko mengi ya kusahaulika kwa wazee hasa katika huduma za afya na maadili.
“Tumeamua kurudi kule tulipotoka, tujaribu kurudisha maadili vijijini, watoto wetu wanaposoma wanabadilika na kusahau jadi yao” amesema Laizer
Kwa upande wake Katibu Mwenenzi wa Chama cha Wazee Wanaume John Sagata akiwasilisha risala ya chama hicho amesema lengo la chama hicho ni kuungana wanaume wazee katika kujadili masuala yanayowahusu ambapo hadi sasa kina jumla ya wanachama 23146 katika mikoa 22 nchini.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Mchungaji Paulo Mpolo amebainisha kuwa, Baraza la Wazee ndio linabeba wazee wote wa kike na wa kiume hivyo amekiomba chama cha Wazee na vyama vingine vyote kushirikiana katika kuwatetea wazee.
“Kazi ya kutengeneza malezi na maadili yoyote ni kazi ya wazee, tulijisahau tukaacha kuwasaidia watoto wetu juu ya maadili yetu ya Kiafrika. Tuamke sasa na tukatae kuitwa tumepitwa na wakati, tusaidie kizazi chetu.” amesema Mzee Mpolo.