Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi CCM (UWT) Bi. Jokate Mwegelo amewataka wazazi kuwa na malezi bora kwa watoto ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili hususani swala la ukatili.
Hayo amesema Leo Oktoba 27, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na viongozi wa (UWT) Jijini Dar es Salaam kwenye ofisi za CCM mkoa kuhusu miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambapo sherehe zake zinatarajiwa kufanyika mwezi ujao visiwani Zanzibar.
Amesema ukatili umekua changamoto kubwa katika jamii hasa kwa wanawake na watoto.
“Wanawake wenzangu hatuwezi kuwa na viongozi wazuri na bora watakaosimama kwenye maadili na muktadha wa nchi yetu tusipowatengeneza viongozi wanaotoka kwenye familia na wanaotoka kwa wazazi kwa hiyo hilo jukumu hatuwezi kulikwepa”amesema Mwegelo
Amesema kuna maeneo mengi wazazi bado hawawatendei haki watoto wao kwa kuwa kikwazo kwa mtoto mpaka kufanyiwa ukatili hivyo amewataka wazazi kufanya majukumu yao ya ulezi kwa watoto wao.
“Sasa hivi tunaona wazazi wanavyowaogopa watoto kuliko watoto kuwaogopa wazazi wakati huko nyuma mtoto akifanya jambo anamuogopa mzazi lakini sio sasa hii inasababisha kuzorotesha maadili na uwezo wa watoto wetu kuwa na uoga na kufanya matendo tofauti yanayoogopeka na jamii”ameongeza
Sambamba na hayo Jokate amesema kamati ya uhamasishaji imeendelea kuwahimiza wanachama wa CCM kujiandaikisha kwenye daftari la kidumu la mpiga kura muda wake utakapowadia
Amesema pia wameendelea kuhamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia mwakani kwenye serikali za mtaa.
“Tunataka sasa hivi wanawake waingie ulingoni ngoma tuicheze sote na sio kuwa wapenzi watazamaji tunataka tupate uwakilishi mzuri”amesema
Aidha ameongeza kuwa (UWT) haitakuwa kikwazo bali itakuwa daraja la kuwawezesha na kuwasemea wanawake wote na mabinti watakaogombea nafasi mbalimbali.
Amesema kufuatia Chama kuweka uwiano wa kugombea kwenye nafasi mbalimbali (UWT) wakati ukifika wa kuchukua fomu za kugombea urais wataenda kumchukulia fomu Rais Samia Suluhu Hassan kwani amejipambanua vyema.
Ziara iliyofanywa na jumuiya hiyo ya wanawake nchi nzima imeweza kuongeza wanachama wapya wa Chama hicho 51431 ambapo pia imefanya mikutano mikubwa ya hadhara 737 katika mikoa 10 lakini pia kupita kwenye kata 750 wilaya 62 ambapo jumla ya miradi 1384 imekaguliwa.
Amesema pamoja na mafanikio waliyoyapata lakini pia wamegundua changamoto ikiwemo baadhi ya vijiji kutokufikiwa na miradi ya umeme na miradi mingine kutokamilika kwa wakati na uhaba wa maji safi na salama kwenye baadhi vijiji.
Aidha amesema kufuatia changamoto hiyo (UWT) imezitaka sekta husika kuhakikisha zinatatua changamoto hizo ikiwemo upatikanaji wa nishati ya umeme ili waweze kukuza na kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Aidha kamati ya utekelezaji imewataka Wabunge wote wa viti maalumu ambao wamepitia UWT kufanya mikutano ya hadhara kwenye maeneo yao kwa lengo la kusikiliza kero zinazowakumba wanawake na kuzitatua na kuyasemea mazuri yanayofanywa na serikali ya Chama cha mapinduzi.
Sambamba na hayo kamati ya utekelezaji ya (UWT) imewataka wanawake waliochukua mikopo ya asilimia 10 kuirejesha kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wengine.