Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milišić, wakisaini Mpango Kazi wa Pamoja wa 2023-2024 wa ushirikaiano kati ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, katika kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi ya Pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma. Anayeshuhudia ni Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milišić, wakionesha hati za Mpango Kazi wa Pamoja wa 2023-2024 wa ushirikaiano kati ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, baada ya kusainiwa katika kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi ya Pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dt. Natu El-maamry Mwamba na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milišić, wakibadilishana hati za Mpango Kazi wa Pamoja wa 2023-2024 wa ushirikaiano kati ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, baada ya kusainiwa katika kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi ya Pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milišić, wakipongezana baada ya kusaini Mpango Kazi wa Pamoja wa 2023-2024 wa ushirikaiano kati ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, katika kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi ya Pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza wakati akifungua Kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi ya Pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milišić, akizungumza wakati wa Kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi ya Pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milišić wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa walioshiriki katika kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi ya Pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
………………
Na. Farida Ramadhani na Saidina Msangi, WF, Dodoma.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa (UN) wamesaini Mpango Kazi wa pamoja wa Mwaka 2023/24 wa ushirikiano wa maendeleo kati ya Serikali na Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Hati za Mpango kazi huo zimesainiwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milišić, katika Kikao cha Pili cha Kamati ya Usimamizi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba amehimiza watekelezaji wote wa Mfumo wa Ushirikiano wa Maendeleo Endelevu wa Umoja wa Mataifa (UNSDCF) zikiwemo Taasisi za Serikali, AZAKi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Umoja wa Mataifa kwa ujumla, kutumia fedha zinazotolewa na washirika wa maendeleo ipasavyo katika kuleta maendeleo nchini.
“Kama wasimamizi wa rasilimali za umma tuna jukumu la kuendeleza ustawi wa wananchi, na kuhakikisha kila shilingi inayotengwa inatumika kwa ufanisi, uwazi, na kwa umakini wa hali ya juu kwa maendeleo ya Taifa” Alisisitiza Dkt. Mwamba.
Alisema Mfumo wa UNSDCF unaweka msisitizo katika ushirikiano thabiti ili kuleta mabadiliko ambapo utekelezaji wake unahitaji ushirikiano endelevu kati ya Tanzania na UN, huku ukiendelea kusisitiza katika maadili, kanuni na viwango vya pamoja vya mfumo wa Umoja wa Mataifa.
“Mkutano huu ni muhimu katika jitihada zetu zinazoendelea za kufikia malengo yetu makubwa yaliyowekwa katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu na hasa baada ya hivi karibuni kuhitimisha Jukwaa la Ngazi ya Juu la Kisiasa la Umoja wa Mataifa lililofanyika Julai 2023, nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine, kama Taifa tuliwasilisha Ripoti ya Tathmini ya Kitaifa ya Hiari ya mwaka 2023 (VNR) kuhusu Utekelezaji wa Ajenda ya 2030 ya SDGs”, alibainisha Dkt. Mwamba.
Aidha, alitoa rai kwa pande zote kuendelea kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura ya 134 (kifungu cha 30) ambayo pamoja na mambo mengine, inatamka kwamba Waziri wa Fedha atakuwa na mamlaka ya kupokea na kwa niaba ya Serikali ruzuku yoyote itakayotolewa kwa Serikali kutoka kwa Serikali yoyote ya kigeni au mtu mwingine, isipokuwa akikasimisha kwa Afisa yeyote wa Umma aliyetajwa kutekeleza kwa niaba ya Serikali makubaliano yoyote au hati nyingine inayohusiana na mkopo, dhamana au ruzuku.
Aliupongeza Umoja wa Mataifa (UN) kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania na kubainisha kuwa msaada unaotolewa na UN umesaidia Serikali katika kutekeleza sera za kiuchumi na mageuzi ili kukuza ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini, na kuboresha ustawi wa kijamii na kiuchumi wa watu ambapo bila msaada huo baadhi ya mipango ya kupunguza umasikini ingechelewa.
Akizungumzia kikao hicho, Dkt. Mwamba alisema kuwa kikao hicho ni hatua muhimu katika dhamira inayoendelea ya kufikia malengo yaliyoainishwa katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milišić, alisema kuwa kutokana na juhudi za pamoja mafanikio makubwa yameweza kufikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja ikiwemo maendeleo ya watu na kujenga mazingira wezeshi.
‘’Tumefanikiwa katika ushirikishaji wa masuala ya kijinsia katika mifumo ya fedha na kutumia kanuni ya kutomwacha yeyote nyuma hasa katika mikakati ya afya. Tulifanikiwa katika kupanua wigo wa utoaji huduma za afya na elimu’’, alisema Bw. Zlatan Milišić.
Aliongeza kuwa walifanikiwa kufanya kazi na Serikali pamoja na washirika wa maendeleo kukusanya rasilimali katika mazingira ya kupunguza usaidizi rasmi wa maendeleo na kufanikiwa kukusanya rasilimali chini ya Mfuko wa Kimataifa (GFTAM), na kuunga mkono mikakati mbalimbali kama vile Mwongozo Maalum wa Kitaifa na mikakati inayohusu Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika na Biashara ya Mtandaoni.
‘’Tumeunga mkono utoaji wa taarifa za makubaliano ya kimataifa ikiwemo kupitia usaidizi kwa Utafiti wa Demografia na Afya (DHS), Sensa ya Watu na Makazi (PHC) na zoezi la Mapitio ya Hiari ya Kitaifa ya 2023’’, aliongeza.
Aidha, alisema kuwa mtazamo wa UN kwa jamii ulisababisha kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa makundi mbalimbali ya watu kuhusu haki, wajibu na wajibu wao katika safari ya kuelekea mafanikio ya maendeleo ya taifa.
Alishukuru kwa ushirikiano ambao UN unapata kutoka kwa Serikali ya Tanzania na kueleza kuwa anatumai ushirikiano huo utaendelea katika ngazi zote, huku akiahidi kuwa UN itaendelea kuunga mkono Serikali katika jitihada za kuleta maendeleo.